Watoto 35 kufanyiwa upasuaji wa moyo kambi maalum ya Mfalme Salman
Na Mwandishi Maalum – JKCI
WATOTO 35 wenye magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo, matundu na mishipa ya damu ya moyo kuziba au kukaa vibaya wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo katika kambi maalum ya matibabu ya moyo inayofanyika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Kambi hiyo ya siku tano iliyoanza Septemba 9,2023 inafanywa na madaktari bingwa wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), kwa kushirikiana na wenzao kutoka Kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu kilichopo nchini Saud Arabia.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt.Sulende Kubhoja, amesema madaktari hao kutoka Kituo cha Mfalme Salman wamekuwa na utaratibu wa kila mwaka kufanya kambi ya matibabu ya moyo na Taasisi hiyo, lengo likiwa kubadilishana ujuzi na kuongeza maarifa.
Dkt. Kubhoja amesema katika kambi wanazofanya na madaktari kutoka Kituo cha Mfalme Salman, watoto wengi wamekuwa wakifanyiwa upasuaji kwa kipindi cha muda mfupi hivyo, kupunguza idadi ya watoto wanaosubiri kufanya upasuaji wa moyo.
“Madaktari wa JKCI tukiwa wenyewe tunaweza kufanya upasuaji mkubwa wa moyo kwa watoto wawili hadi watatu kwa siku, lakini wakija hawa wenzetu kwasababu wanakuja wengi ushirikiano unakuwa mkubwa na kutuwezesha kutoa huduma ya upasuaji wa moyo kwa watoto watano hadi sita kwa siku,” amesema Dkt. Kubhoja.
Dkt.Kubhoja amewaomba wazazi wenye watoto wenye magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo kujitokeza kwa wingi ili weweze kupatiwa huduma za matibabu kwa wakati.
Kwa upande wake daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto kutoka Kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu kilichopo nchini Saudi Arabia, Mohammed Shihata, amesema ujio wao hapa nchini ni kampeni ya kutoa huduma za upasuaji wa moyo kwa watoto wenye magonjwa ya moyo.
Dkt.Shihata amesema madaktari kutoka Kituo cha Mfalme Salman wanapenda kufanya kazi na wataalamu wa afya wa JKCI kwa sababu ya ukarimu wa watu wa Tanzania, uwajibikaji wa wataalamu wa afya wa JKCI na ujuzi uliopo kwa wataalam hao.
“Kambi zetu za matibabu ya moyo kwa watoto hapa Tanzania ni moja ya kambi ambazo zinakuwa zimeratibiwa vizuri hivyo, mara nyingi hutupa nafasi ya kuanza kazi siku ya kwanza tunayofika,” amesema Dkt.Shihata.
Dkt. Shihata amesema ujio wa wataalamu hao umekuja na vifaa tiba vilivyotolewa na Kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu kilichopo nchini Saudi Arabia kwa ajili ya kuwafanyia upasuaji watoto 35 wenye magonjwa ya moyo.
Mzazi ambaye mtoto wake anatarajiwa kufanyiwa upasuaji katika kambi hiyo kutoka mkoani Kigoma, Merry Japhet, amesema anamshukuru Mungu kwa mwanaye kuwekwa kwenye idadi ya watoto wakataopatiwa matibabu katika kambi hiyo kwani, ni matamanio yake kuona mtoto wake anapona kabisa tatizo la moyo.
“Mungu akijalia mwanangu atafanyiwa upasuaji wa moyo, nilimzaa akiwa na tundu kwenye moyo na mishipa yake ya damu ikiwa imesinyaa, akiwa bado na miezi michache baada ya kuzaliwa alikuwa akiumwa mara kwa mara, nilimpeleka hospitali wakaniambia ana tatizo la nimonia na kumchoma sindano za nimonia, lakini hakupona,” amesema Merry.
Merry amesema siku moja akiwa anamuogesha mwanaye, aliona upande wa kushoto wa kifua umevimba hivyo, kuamua kumpeleka Hospitali ya Wilaya na kugundulika kuwa, ana shida ya moyo hivyo, kuanza kufuatilia matibabu ya moyo katika Hospitali ya Bugando, Benjamini Mkapa na baadaye kupewa rufaa kufika JKCI.
“Namshukuru Mungu nilivyofika hapa JKCI nimepokelewa vizuri, mtoto amepatiwa tiba kwa kipindi cha mwezi mmoja hadi sasa anaendelea vizuri, ndiyo wakaona ni wakati sasa afanyiwe upasuaji wa moyo kurekebisha changamoto alizonazo,” amesema Merry.
No comments