PSSSF yapunguza muda wa kusubiri mafao
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa PSSSF, CPA Hosea Kashimba
MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), umesema utaendelea kuimarisha huduma zake kwa wateja ili kuongeza ufanisi na kupunguza urasimu na muda wa malipo kwa wanufaika wa mfuko huo.
Hayo yameelezwa Agosti 31, 2023 na CPA Hosea Kashimba, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa PSSSF, wakati wa Mkutano wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, PSSSF na wahariri wa Vyombo vya habari Jijini Dar es Salaam.
Amebainisha kuwa, kwa sasa Mfuko huo umepunguza muda wa malipo kwa pensheni ya kila mwezi, ikiwa ni wastani wa shilingi billioni 67 hulipwa kwa wastaafu kila ifikapo tarehe 25 ya mwezi husika ambalo ni ongezeko la asilimia 100 ukilinganisha na kiasi cha wastani wa shilingi bilioni 34 wakati mfuko huo unaanzishwa.
Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa, kwa sasa Mfuko huo umepunguza muda wa kusubiri mafao kutokana na kwamba, Mfuko unalipa ndani ya siku 60, kwa mujibu wa sheria, kabla ya kuanzishwa kwa Mfuko huo wastaafu wengine walitumia zaidi ya miaka 3 kusubiri mafao yao, Mfuko tangu kuanzishwa kwake umefanikiwa kulipa madai mbalimbali yaliyorithiwa kutoka kwenye Mifuko iliyounganishwa.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile |
Kiasi cha Shilingi trilioni 1.03 kililipwa ndani ya miaka miwili kwa zaidi ya wanufaika 10,273, pia thamani ya Mfuko imeongezeka kwa asilimia 27.76 kutoka shilingi trilioni 5.83 hadi shilingi trilioni 8.07, kwa sasa wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii wanalipwa kwa kanuni inayofanana,”amesema CPA Kashimba.
Mkurugenzi huyo ameweka wazi kwamba, hadi sasa kiasi cha shilingi trilioni 8.88 kimelipwa kwa wanufaika na wengi wao wakiwa ni wastaafu katika makundi ya Mafao ya Uzeeni/Kustaafu, shilingi trilioni 4.63 (asilimia 52.19), Pensheni ya kila mwezi shilingi trilioni 3.31 (asilimia 37.26), Mafao ya Kifo shilingi billion 461.72 (asilimia 4.69), Mafao ya kuacha kazi shilingi billion 350.99 (asilimia 3.95), Mafao ya Elimu shilingi billioni 5.56 (asilimia 0.06), Mafao ya uzazi shilingi billion 57.76 (asilimia 0.65), Mafao ya Ugonjwa shilingi billion 7.97 (asilimia 0.09), Mafao ya kukosa ajira, shilingi billioni 5.80 (asilimia 0.07), Malipo ya Michango shilingi billion 92.24 (asilimia 1.04)
Mfuko huo umeendelea na shughuli za uwekezaji katika miradi ya ubia ili kujiongezea mapato, ambapo imebainishwa kuwa uwekezaji huo utaongeza fursa ya kuongeza ukwasi katika Taasisi za fedha na kuwezesha wananchi kupata mikopo kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo na kiuchumi, kuongeza ajira, kodi serikalini na kukuza mitaji
CPA Kashimba amesema miongoni mwa miradi ya ubia na wawekezaji wengine kwenye Sekta ya Viwanda ni Kiwanda cha Kimataifa cha Bidhaa za Ngozi cha Kilimanjaro kilichopo Moshi mkoani Kilimanjaro, PSSSF (asilimia 86) na Jeshi la magereza (asilimia 14).
Awamu ya Kwanza ya Kiwanda hicho ilizinduliwa Oktoba, 2020, Machinjio ya Kisasa ya Nguru Hills: PSSSF (asilimia 39), Eclipse Investment LLC (asilimia 46), na Busara Investment LLP (asilimia15), Kiwanda cha kuchakata Tangawizi cha Mamba Myamba, PSSSF (asilimia 65) na Ginger Growers Rural Cooperative Society (MGGRCS) (asilimia 35), na Kiwanda cha Chai cha Mponde PSSSF (asilimia 42), WCF (asilimia 42), na ofisi ya Msajili wa Hazina (asilimia 16).
“Mfuko umefanikiwa kuongeza thamani ya uwekezaji kwa asilimia 23.5, kutoka shilingi trilioni 6.40 hadi shilingi trilioni 7.92, wastani wa ongezeko la asimilia 4 kila mwaka, lakini pia mfuko umepata mapato yatokanayo na uwekezaji ya wastani wa asilimia 85 kwa mwaka, pamoja na kuwaunganisha Wafanyakazi wote waliotoka kwenye Mifuko minne iliyokuwa na utamaduni tofauti, kuandikisha Wanachama wapya 140,162 kwa wakati ikiwa ni waajiriwa wa Serikali na Taasisi zake, ambapo kwa sasa idadi ya wanachama kwenye Mfuko ni 731,183, wanaume wakiwa ni 434,667 na wanawake ni 296,516,” amefafanua CPA Kashimba.
Mfuko huo umejipanga kuhakikisha huduma zote zinafanyika kwa njia ya mtandao ifikapo 2024, ambapo kwa sasa ni asilimia 90, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) inatumiwa na Mfuko huo katika kazi zake lakini pia kuwekeza zaidi katika kuendeleza rasilimali watu ili kuongeza ubunifu na ufanisi katika utendaji, kuimarisha ushirikiano wa kikazi na Taasisi washirika katika utoaji wa huduma, kuendelea kupunguza muda unaotumika kulipa Mafao kutoka siku sitini za sasa hadi kufikia siku zisizozidi 30.
Mfuko wa PSSSF, ulianzishwa mwaka 2018 kupitia sheria ya Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi, Sura 371, ambapo ni matokeo ya ya kuunganishwa kwa Mifuko ya GEPF LAPF, PPF, PSPF, ili kuleta uendelevu wa Mifuko, kuondoa ushindani uliokuwa hauna tija kwa Mifuko kushindania wanachama wachache waliokuwa wanaingia katika soko la ajira ikilinganishwa na idadi ya Mifuko iliyokuwepo.
Maofisa kutoka mfuko wa PSSSF wakiwa katika kikao hicho.
No comments