JKCI Dar Group yaboresha huduma ya dharura
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt.Peter Kisenge akiangalia namna ambavyo wataalamu wa afya wa JKCI Dar Group wakifanya mazoezi kwa vitendo ya namna ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura, wakati wa uzinduzi wa Kitengo cha wagonjwa wa dharura katika hospitali hiyo leo Agosti 31,2023 jijini Dar es Salaam |
HUDUMA za dharura kwa wagonjwa zimeboreshwa kwa kuwekeza vifaa vya kisasa na wataalamu mabingwa wa kutoa huduma hizo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Hospitali ya Dar Group.
Kitengo hicho cha dharura Hospitali ya JKCI Dar Group sasa kimeimarishwa kwa kuwekeza vifaa vyenye gharama ya shilingi milioni 760, ambavyo ni mashine za kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiograph – ECHO) na mashine za kiwango cha juu za magonjwa ya dharura Advanced Cardiac Monitors, Defibrillator, Emergency Trolley na Ventilator.
Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 31,2023 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt.Peter Kisenge, amesema tangu serikali ilivyoipa dhamana JKCI kusimamia Hospitali ya JKCI Dar Group imeendelea kuimarisha huduma na kuongeza vifaa vya kisasa katika kitengo cha magonjwa ya dharura.
“Tumeimarisha kitengo cha dharura kwa kuwekeza madaktari bingwa wanaotoa huduma kwa wagonjwa mahututi wawili na kutoa mafunzo ya namna ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura kwa wataalamu wengine wa afya wanaofanya kazi katika Hospitali hii,” amesema Dkt. Kisenge.
Kisenge ambaye pia ni Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo amemshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mchango wake katika uboreshwaji wa hospitali hiyo kwa kuendelea kuwekeza vifaa vya kisasa hivyo, kusogeza huduma karibu na wananchi.
“Katika mwendelezo wa kusogeza huduma kwa wananchi, JKCI inaendelea kupeleka huduma mikoani,hadi sasa tayari tumetembelea mikoa 11 na kuona watu zaidi ya 7,000 ambao wengi wao hawakuwahi kupata huduma za kibingwa za matibabu ya moyo.
"Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt.Angella Muhozya, amesema tangu kuanzishwa kwa kitengo cha dharura katika Hospitali ya JKCI Dar Group Desemba mwaka jana, idadi ya wagonjwa imekuwa ikiongezeka kutoka wagonjwa watatu hadi watano, ambapo sasa kitengo kinapokea wagonjwa tisa hadi 15 wanaohitaji huduma za dharura.
“Kutokana na wingi wa wagonjwa, tumeona kuna ulazima wa kuongeza vitendea kazi na wataalamu wabobezi ili tunavyokuza huduma, tuwe na uwezo wa kumudu mahitaji yote yanayohitajika kutoa huduma kwa wagonjwa wa dharura ndiyo maana Taasisi ikawekeza vyakutosha,” amesema Dkt.Angella
Dkt.
Angella amesema huduma ya magonjwa ya dharura hapo awali ilikuwa ikitolewa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) pekee, lakini baada ya wataalamu wa afya kupata mafunzo ya kutoa huduma hiyo, huduma za dharura zinaanza kupatikana maeneo mengine kama ambavyo sasa inapatikana Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete.
“Kwasasa JKCI kuwa na wataalamu wabobezi wa kutoa huduma kwa wagonjwa wa dharura ni hatua kubwa kwani, wataalamu hao kwa nchi nzima si zaidi ya 15 hivyo, kuifanya taasisi yetu kuwa na viwango vinavyokubalika kimataifa,” amesema Dkt.Angella.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter
Kisenge akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa kitengo cha
wagonjwa wa dharura kilichopo Hospitali ya JKCI Dar Group leo Agosti 31,2023 jijini Dar es
Salaam
Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt.Angella Muhozya akielezea huduma zinazotolewa katika kitengo cha wagonjwa wa dharura wakati wa uzinduzi wa kitengo hicho kilichopo Hospitali ya JKCI Dar
Group leo jijini Dar es Salaam.
Daktari wa usingizi na mkuu wa timu ya kuratibu jinsi ya kuokoa wagonjwa wa dharura wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Faraji Lydenge akimuonesha mtaalamu wa afya wa Hospitali ya JKCI Dar Group namna ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura, wakati wa uzinduzi wa kitengo cha wagonjwa wa dharura katika hospitali hiyo leo Agosti 31,2023 jijini Dar es Salaam. Picha zote na JKCI
No comments