Header Ads

ad

Breaking News

TAKUKURU YAWABURUZA MAHAKAMANI WALIMU WAWILI NA WALIOKUWA WATUMISHI HAI

Joyce Anael, Hai
 
TAASISI ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Kilimanjaro, imewafikisha mahakamani  aliyekuwa Afisa  utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Faraja Kingdom Ndatu na aliyekuwa Mchumi wa Halmashauri hiyo Isaiah Michael Bayege. 
engine waliounganishwa katika kesi hiyo ni Alizan Abdallah Mruma ambaye ni mwalimu wa shule ya sekondari Rau iliyoko manispaa ya Moshi na Athman Abdul Mbowe  mwalimu wa Shule ya sekondari Udoro iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Hai. 
 Washtakiwa hao kwa pamoja wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na makosa ya kula Njama, kughushi, kuwasilisha nyaraka za udanganyifu na kujipatia kiasi cha fedha cha shilingi Milion Thelathini na Tano (35,000,000)kwa njia ya udanganyifu  kutoka  Benki ya CRDB Tawi la Hai. 
Mwendesha mashtaka wa Takukuru, Barry Galinoma  aliwafikisha watuhumiwa hao mahakamani juzi mbele ya hakimu mfawidhi wa mahakama ya Wilaya ya Hai Mheshimiwa Anord Kyirakyando. 
 Katika kesi hiyo ya Jinai Namba ECC.11/2017,mwendesha Mashtaka wa Takukuru alidai kuwa washtakiwa hao kwa pamoja, walikula njama na kutengeneza vitambulisho kwa kutumia majina ya watumishi waliostaafu katika Halmashauri ya Wilaya ya Hai na kisha wakabandika picha za Alzan Abdalla Mnduma na Athuman Abdul Mbowe kwenye vitambulisho hivyo. 
Baada ya kutengeneza vitambulisho hivyo mshtakiwa Faraja na Bayege, waliandaa Check Namba za udanganyifu na kasha kufanya udhamini kwa Alizan na Athuman katika Benki ya CRDB na kuonyesha kuwa watajwa kwenye vitambulisho hivyo vya kughushi ni watumishi wa Halmashauri na kushauri wapewe mkopo na Benki.
 Imedaiwa mahakamani hapo washakiwa hao walitenda kosa hilo kati ya Januari 2014 na octoba 31,2015 katika Halmashauri ya Wilaya ya Hai na kutokana na udanganyifu huo washtakiwa hao waliweza kujipatia kiasi cha  sh. milioni 35. 
Hata hivyo washtakiwa Alizan Mruma na Thuman Mbowe wamekana mashtaka hayo na kwamba Mbowe yuko nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya Dhamana huku mshtakiwa Alizan Mruma akipelekwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya Dhamana.

Washtakiwa Faraja Ndatu na Isaiah Bayege, hawakuwepo mahakamani hapo wakati mashtaka hayo yakisomwa ambapo mahakama ilitoa hati ya wito ili waweze kufika mahakamani hapo kusomewa mashtaka yanayowakabili, na kwamba kesi hiyo itatajwa tena mahakamani hapo Oktoba 3, 2017.


No comments