SERIKALI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA SEKTA BINAFSI KUFANIKISHA TANZANIA YA VIWANDA.
Mwandishi Wetu-MAELEZO
Waziri wa Fedha na Mipango
Dk. Philip Mpango amesema serikali inathamini mchango wa sekta binafsi na
itaendelea kushirikiana nayo katika kuhakikisha azma ya Tanzania ya viwanda
inafikiwa.
Dk. Mpango amesema
hayo Jijini Dar es Salaam leo alipokuwa akizindua kitabu cha Safari ya Tanzania
kuelekea katika Uchumi wa Viwanda 2016- 2056, kilichoandikwa na watanzania
wazalendo Bw. Ali Mufuruki, Gilman Kasiga na Moremi Marwa.
"Kitabu hiki ni kama
mkombozi kwa sisi watunga sera kwani kitatusaidia katika kuyafanyia kazi
mapendekezo ambayo yametolewa ili kuhakikisha Tanzania ya viwanda inawezekana,
nimewaelekeza pia Tume ya Mipango na Idara ya sera katika Wizara ya Fedha
kuchukua mapendekezo ambayo wataona yataisaidia serikali katika kutekeleza azma
yake ya kuendeleza viwanda," alisema Dk. Mpango
Ali Mufuruki mmoja wa watunzi wa kitabu hicho
amesema wameamua kuunganisha mawazo yao pamoja na kutumia utaalamu na uzoefu
wao katika masuala mbalimbali ya maendeleo na uchumi ili kuisaidia serikali
kuweza kuondokana na uchumi unaotegemea kilimo na hatimaye kuwa nchi ya
viwanda.
‘’Kuna changamoto
nyingi zinazozikabili nchi zinazoendelea ikiwemo ukosefu wa utaalamu katika kilimo
cha kisasa, ukosefu wa mitaji pamoja na kutokuwa na teknolojia ya kutosha hivyo
kwa kuwa azma ya Mh. Rais Dkt. John Pombe Magufuli ni kuwa na nchi ya uchumi wa
kati unaotegemea viwanda, tukaona tumuunge mkono katika kutimiza ndoto hiyo kwa
kuandika kitabu hiki’’ amesema Mufuruki.
Mufuruki amesema
kuna mambo mengi mazuri ya kulisaidia taifa ambayo yameainishwa katika kitabu
hicho hivyo ni vyema watanzania wa kawaida, wasomi, wachumi na hata wawekezaji
wakakisoma ili kuona kila mmoja katika nafasi yake anawezaje kuisaidia nchi
kutoka hapa ilipo na kufikia katika malengo iliyojiwekea.
Gilman
Kasiga ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya General Electric katika ukanda wa
Afrika Mashariki, amesema ni vyema Tanzania ikawekeza katika masomo kwa
kutambua vipaumbele kama inavyofanya nchi ya Ujerumani ambapo sio kila
anayesoma ni lazima afikie ngazi ya shahada ndipo aonekane anaweza kuleta
mchango katika maendeleo.
Kasiga amesema
asilimia 70 ya wanaomaliza shule hapa nchini wanakimbilia kusoma shahada na
kusahau kwamba kuna masomo mengine katika ngazi za astashahada na cheti ambayo
kama yakifundishwa kwa umakini na kwa kuzingatia fani husika yanaweza kuzalisha
wataalamu wengi ambao wataisaidia nchi kupiga hatua kimaendeleo na pia wao
kupata ajira kwa urahisi katika viwanda.
Amesema elimu ya vyuo
vikuu ni ya kuandaa wasimamizi yaani mameneja na sio watendaji au wafanya kazi
na mafundi hivyo ameshauri mitaala ya vyuo iendane na ukuaji wa viwanda ili
wataaalamu hao waweze kutumia taaluma zao katika kulitumikia taifa.
Mwisho.
No comments