ZANZIBAR KUWABANA KISHERIA WAVUTAJI SIGARA HADHARANI

Katibu Mkuu Wizara ya Afya
Zanzibar Bi. Asha Ali Abdallah akizungumza na walikwa katika uzinduzi wa
kanuni ya udhibiti wa tumbaku uliofanyika ukumbi wa Wizara ya Afya
Zanzibar. Kulia mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani Dr. Matthieu
Kamwa.

Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Bi.
Harusi Said Suleiman akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kitabu cha
kanuni ya kuzibiti matumizi ya tumbaku Zanzibar (kushoto alieshika
kitabu) ni Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani Dr. Matthieu Kamwa.

Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Bi.
Harisi Said Suleiman na Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani Dr.
Matthieu Kamwa wakionyesha Kitabu cha kanuni ya kuzibiti matumizi ya
tumbaku Zanzibar kilichozinduliwa leo Wizara ya Afya.

Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Bi.
Harusi Said Suleiman wa (katikati) katika picha ya pamoja na viongozi
wa WHO pamoja na watendaji wa Wizara ya Afya Zanzibar.
Picha na Makame Mshenga.
……………………………………………………………………
Na Mwashungi Tahir – Maelezo
Wizara ya Afya imezindua kanuni
ya udhibiti wa matumizi ya Tumbaku ikiwa ni mkakati wa kupambana na
ongezeko la Matumizi ya Tumbaku kwa jamii ya Zanzibar.
Hafla ya uzinduzi huo imefanywa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Harusi Saidi Suleiman huko Wizara ya Afya mnazi mmoja.
Akizungumza katika hafla hiyo
Naibu huyo amesema jamii ya kizanzibari inakabiliwa na changamoto kubwa
ya matumizi ya tumbaku ikiwemo uvutaji wa sigara.
Amesema Sigara ni bidhaa halali
inayoingizia Serikali mapato kupitia kodi, hata hivyo mbali na mapato
yanayopatikana , matumizi yake yamethibitika kuwa ni athari kubwa mno
kwa mtumiaji pamoja na wanaomzunguka .
“Ifahamike kuwa tumbaku ina aina
nyingi ya sumu ikiwemo NIKOTIN ambayo inasababisha uraibu na
husafirishwa kwa njia ya mzunguko wa damu na kuathiri sehemu mbali mbali
za mwilini” alisema Naibu huyo.
Alisema tafiti zilizofanywa
ulimwenguni zinafahamisha kuwa matumizi ya tumbaku ikiwemo uvutaji wa
sigara hupelekea kupata maradhi yasiyoambukiza ikiwemo Saratani za
mapafu, kinywa, shingo ya kizazi , ugonjwa wa shinikizo la damu na
kisukari .
Aliongeza kuwa matumizi yake
huathiri pia mfumo mzima wa mishipa ya damu, maradhi sugu ya kuziba njia
ya hewa kusababisha maradhi ya kiharusi.
Akielezea kuhusu Utafiti
uliofanyika Zanzibar mwaka 2011 Naibu huyo alisema asilimia 7.3 ya watu
katika jamii ni watumiaji wa Sigara na bidhaa zitokanazo na tumbaku, na
kwa upande wa wanafunzi tafiti ndogo zilizofanyika imebainika skuli
zaidi ya nane zilizomo wilaya ya mjini asilimia 9.5 ya wanafunzi
wanatumia bidhaa zitokanazo na tumbaku ikiwemo sigara.
Akizitaja changamoto katika jamii
alisema ni matumizi holela ya tumbaku hususan uvutaji wa sigara katika
maeneo ya uwazi kama vile majengo yanayotoa huduma za kijamii, maeneo
ya burudani, sokoni, viwanja vya mpira.
Naibu huyo alieleza kuwa Zanzibar
inashuhudia watoto chini ya umri wa miaka 18 wakishirikishwa kwa njia
moja au nyengine katika matumizi hayo na kwamba ipo haja wazazi na
walezi kuwa na hadhari kwa watoto wao.
Ameviomba vyombo vya habari na
vyombo vya sheria kuzipitia na kuzisimamia kanuni hizo ili kuweza
kukabiliana na changamoto za matumizi hayo ikiwa ni pamoja na
kuhakikisha mtu atakayeuza bidhaa ya tumbaku ikiwemo sigara lazima
bidhaa hiyo iambatane na onyo la afya liililochapishwa kwa wino mwekundu
na inayosomeka vizuri.
Kanuni hizo pia zinakataza mtu
yeyote chini ya umri wa miaka 18 kutoruhusiwa kujishughulisha na kuuza
sigara au kushiriki katika bidhaa ya tumbaku na kanuni inakataza
kudhamini na kuhamasisha bidhaa hii ikiwa nchini au nje ya nchi kupitia
vyombo vya habari na matangazo yanayohamasisha matumizi ya tumbaku.
Nae Mwakilishi wa Shirika la Afya
duniani (WHO) Dr. Matthieu Kamwa amesema tumbaku ni miongoni mwa
bidhaa zinazoongoza kusababisha vifo kwa watumiaji wake ambapo zaidi ya
watu million saba hufariki duniani kote kutokana na matumizi yake.
Mwakilishi huyo amesema Tumbaku
ni janga kubwa ambalo linagharimu uchumi wa dunia ambapo takriban dola
za Marekani Tirion 1.2 hutumika kwa ajili ya matibabu ya watumiaji wa
tumbaku.
Ameongeza kuwa Shirika la afya
ulimwenguni litaendelea na mashirikiano yake na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar katika kutengeneza kanuni zake dhidi yamatumizi ya tumbaku .
“Malengo endelevu ya dunia ni
kuona dunia iko salama dhidi ya matumizi ya tumbaku ifikapo 2030 na ni
jambo linalohitaji mashirikiano ya kila mdau katika kuhakikisha
wanaepukana na matumizi hayo” alisema Kamwa.
Kwa upande wake Katibu mkuu wa
wizara ya Afya Asha Ali Abdullah akizungumza katika uzinduzi huo alisema
tumbaku ni miongoni mwa Madawa ya kulevya hivyo ameomba elimu itolewe
ili watumiaji waelewe athari zake hasa kwa vijana ambao ni nguvu kazi ya
taifa la kesho.
No comments