Friday, July 21, 2017

Wakulima watakiwa kuzingatia kilimo cha utafiti

Mkuu wa Wilaya ya Nzega mkoani Tabora, Geofrey Ngupula akizungumza na maofisa ugani na waandishi wa habari wilayani humo jana (hawapo pichani),  wakati akifungua mafunzo ya siku moja ya maofisa ugani yaliyoandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kupitia Jukwaa la Bioteknojia (OFAB). Kulia ni Katibu wa Umoja wa Wanawake Tanzania wa CCM (UWT),, wilayani humo, Arafa Njechele na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, Kiwele Michael. (PICHA NA DOTTO MWAIBALE)

                                                         Dotto Mwaibale, Nzega

TANZANIA ya Viwanda itafanikiwa kwa  kuzingatia kilimo cha kitafiti na kuachana na kilimo cha mazoea.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Nzega mkoani Tabora, Geofrey Ngupula wilayani humo jana wakati akifungua mafunzo ya siku moja ya maofisa ugani wa wilaya hiyo yalioandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kupitia Jukwaa la Bioteknojia (OFAB),  yenye lengo la kuwakumbusha wataalamu hao wa kilimo nafasi yao pamoja na kuwapatia mbinu mpya za kisasa katika kulima mazao ya Mihogo,Pamba na Viazi lishe katika kuelekea serikali ya viwanda.

Amesema inaaminika zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania ni wakulima, zaidi ya robo tatu wakilima kimazoea na kutokana na mabadiliko ya tabia nchi kilimo kinaendelea kumdidimiza mkulima  na kukifanya kilimo kuajiri idadi kubwa ya mafukara

Alisema Teknolojia ya uhandisijeni  inafanya vizuri duniani kote hivyo nchi inatakiwa kuitekeleza ili kuyafikia mapinduizi halisi ya kilimo katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi yanayo leta ukame na magonjwa na wadudu kuwa sugu.

Katika hatua nyingine Ngupula amewataka maofisa ugani kubadilika ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia ya kilimo katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za kilimo.

Akizungumza wakati akitoa mada kwa maofisa ugani hao kuhusu matumizi ya Bioteknolojia katika kilimo, Mshauri wa masuala ya bioteknolojia kutoka Jukwaa la Bioteknolojia OFAB, Dk.Nicholaus Nyange amesema teknolojia hiyo imeleta mapinduzi ya kilimo kwa nchi ambazo imeanza kuitumia hivyo wakati sasa ufike wa kuanza kuitumia hapa nchini.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Costech,Bestina Daniel amesema mafunzo hayo ni moja ya utekelezajiwa kazi za COSTECH za kuwawezesha wakulima na wagani katika kutumia mbinu na teknolojia bora za kilimo kwenye uzalishaji ili kuongeza tija na kupunguza umasikini kwenye kaya.


Amesema Costech ndio wenye dhamani ya kuishauri Serikali kwenye masuala yote yanayohusu Sayansi na Teknolojia hivyo pale kunapotokea teknolojia na mbinu nzuri ambazo zinaweza kuleta mageuzi kwenye uzalishaji kwa wakulima hutafuta mbinu mbalimbali za kuzifikisha kwa wahusiaka.

Ameongeza kuwa  ili kufikia kwenye uchumi wa viwanda lazima malighafi za kutosha ziwepo ili kulisha viwanda hivyo na kuzalisha bidhaa hivyo mazao hayo ambayo Costech inayahamasisha yatasaidia sana katika kulisha viwanda vya nguo,usindikaji wa mihogo na viazi lishe ambavyo vina umuhimu mkubwa kwenye kuongeza lishe na usalama wa chakula.


Mafunzo hayo ya siku moja kwa maofisa ugani hao yanalenga kuwapatia mbinu bora za uzalishaji wa mazao ya Mihogo,Viazi lishe pamoja na Pamba na nafasi ya matumizi bioteknolojia kwenye kuongeza uzalishaji na kutatua changamoto za kilimo kama magonjwa,wadudu na matatizo ya mabadiliko ya tabia nchi.





No comments:

Post a Comment