Wazir Junior amwaga wino kuitumikia Azam FC miaka miwili
UONGOZI
wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, unapenda
kuwataarifu mashabiki wa soka nchini kuwa leo umefanikiwa kuingia
mkataba wa miaka miwili na mshambuliaji anayekuja kwa kasi hivi sasa
nchini, Wazir Junior.
Junior aliyependekezwa na Kocha Mkuu Aristica Cioaba, anakuwa
mchezaji wa kwanza kusajiliwa na timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao
2017-18, ambapo alikuwa straika kinara wa Toto African ya Mwanza msimu
uliopita, akiwa mfungaji wao bora kwa mabao sita aliyofunga.
Zoezi la kuingia mkataba kwa pande hizo mbili limefanyika leo mchana
kwenye Ofisi za Mzizima, zilizopo barabara ya Nyerere, Dar es Salaam, na
kusimamiwa na Meneja Mkuu wa Azam FC, Abdul Mohamed, aliyekuwa sambamba
na viongozi wengine Meneja wa timu, Phillip Alando na Ofisa Habari,
Jaffar Idd.
Azam FC ambayo imeanzisha falsafa ya kutengeneza timu ya muda mrefu
yenye wachezaji vijana wenye vipaji pamoja na kuwekeza ipasavyo kwenye
kituo chake cha kukuza vipaji ‘Azam Academy’ kwa kupandisha wachezaji
bora, inaamini ya kuwa ujio wa mshambuliaji huyo utaongeza zaidi makali
kwenye eneo la ushambuliaji.
Mshambuliaji huyo anaungana na washambuliaji wengine kikosini, Yahaya
Mohammed, Shaaban Idd, Samuel Afful na Yahaya Zaidi, aliyepandishwa
kwenye timu kubwa kwa ajili ya msimu ujao akitokea katika kituo cha
kukuza vipaji vya ‘Azam Academy’.
Wachezaji wengine ambao tayari wameongezwa kwenye timu kubwa kuelekea
msimu ujao wakitokea kituo hicho, ni mabeki Abbas Kapombe, Abdul Haji,
Godfrey Elias, kiraka Ramadhan Mohamed na kiungo Stanslaus Ladislaus.
Kwa taarifa zaidi za kina, kuhusiana na habari mbalimbali za Azam FC
kuelekea kipindi hiki cha usajili, unaombwa kuendelea kufuatilia vyanzo
vya rasmi vya habari vya timu hiyo kwenye mtandao wa kijamii wa facebook
‘Azam FC’, instagram ‘azamfcofficial’ na tovuti ya ‘www.azamfc.co.tz’.
No comments