Viongozi wa kisiasa watakiwa kuwa wavumilivu

Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum.
………………………………………………………..
Na Sheila Simba-MAELEZO
Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Alhad Mussa Salum ametoa wito kwa viongozi wakisiasa Nchini,
kuwa wavumilivu ili kulinda Amani ya Nchi.
Sheikh Alhad ameyasema hayo leo,
ofisini kwake, jijini Dar es Salaam ambapo amewataka viongozi hao kutii
mamlaka iliyoko kwani mamlaka hiyo imewekwa na Mungu na hivyo ni vema
kutafuta njia nyingine kumaliza matatizo yanapotokea.
“Ipo haja ya kuvumiliana kwa ajili
ya Taifa letu, kwani yanapotokea machafuko waathirika wakubwa ni
wanawake, watoto na vijana wetu ambao wanaweza kupata madhara makubwa na
hata kupoteza maisha’’alisema Alhad
Akizungumzia maandamano ya ukuta
yaliyopangwa kufanyika Septemba Mosi, amesema kuwa kauli ya kuzuia
maandamano hayo imetolewa na Rais wa Nchi na kuomba kauli hiyo kuchuliwa
kwa uzito wa kipekee, kwani busara ni kusikiliza mamlaka imesema nini
na kutii kauli hiyo ya Rais.
“Nawashauri Watanzania wenzangu,
viongozi wangu wa kisiasa jambo hilo si vyema tukashiriki kwani kutotii
mamlaka ni dhambi ndivyo vitabu vya dini vinanavyosema,’’ alifafanua
Sheikh Alhad
Ameongeza kuwa suala la kulinda
amani ni la watanzania wenyewe kwa kusaidiana na Jeshi la Polisi ili
kuhakikisha amani inaendelea kuwepo, kwani ni rahisi kupoteza amani
tuliyonayo lakini ni vigumu kurudisha amani.
Amesema kuwa vijana wasikubali
kutumika kwa maslahi ya watu wengine kwani kufanya hivyo ni kushindana
na dola na kutolea mfano wa machafuko yanayoendelea kwa baadhi ya Nchi
Duniani na kupelekea mataifa hayo kutokalika kutokana na vurungu za
kisiasa.
Aidha amewaomba vijana kutokubali
kulitia doa Taifa, kwani Tanzania inafahamika ni kisiwa cha Amani
Duniani na inapaswa kulinda heshima hiyo ili kuendelea kutunza amani ya
Watanzania wote bila kujali tofauti za kisiasa.
Amewaomba viongozi hao wa kisiasa
kuwasilisha malalamiko yao kwa njia tofauti kwani Serikali iliyopo
madarakani ni sikivu na ipo kwa ajili ya wananchi wote.
No comments