Baraza Kuu la Uongozi (CUF) lamsimamisha Uanachama LIPUMBA na Wenzake 10
Ndugu Waandishi wa habari,
Awali
ya yote naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai
na uzima wa afya na tukaweza kukutana hapa asubuhi hii ya leo.
Tunamshukuru Mwenyezi Mungu pia kwa kuijaalia nchi yetu kuendelea kubaki
katika hali ya amani na utulivu licha ya matatizo mengi yanayotukabili.
Pili,
nichukue fursa hii kukushukuruni nyinyi waandishi wa habari kwa
kuitikia wito wetu na kuja kutusikiliza. Ni imani yangu kuwa kama
ambavyo mmekuwa mkitupa mashirikiano mazuri katika kuwafikishia wananchi
yale ambayo chama chetu kupitia kwenu kimekuwa kikiyatolea taarifa, kwa
uzito wa kipekee taarifa hii nayo mtawafikishia Watanzania wote kupitia
vyombo vyenu vya habari.
Ndugu Waandishi wa habari,
Tumewaita
leo hii kuwaeleza juu ya maazimio ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la
Taifa katika kikao chake cha dharua kilichofanyika jana, Jumapili ya
tarehe 28/08/2016 Katika ukumbi wa Makao Makuu ya Chama, ofisi za Vuga.
Kikao
hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti wa muda Mhe, Hamidu Hassan Bobali,
Mbunge wa Jimbo la Mchinga kilihudhuriwa wa Wajumbe 46 katika ya Wajumbe
60.
Ndugu Wandishi wa Habari,
Kama
mnavyojua tarehe 21/08/2016 Chama Cha Wananchi – CUF kilikuwa na
Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa uliofanyika katika ukumbi wa Blue Pearl,
Ubungo Plaza, Dar es Salaam. Mkutano huo ulikuwa na agenda mbili kuu,
ambazo ni:-
1. Kupokea barua ya Profesa Ibrahim Haruna Lipumba ya kujiuzulu nafasi yake ya uenyekiti ya tarehe 05/08/2015; na
2.
Kufanya Uchaguzi wa kujaza nafasi zilizo wazi - Mwenyekiti Taifa,
Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wanne wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.
Kufuatia
hujuma za makusudi zilizoandaliwa kwa mashirikiano ya maadui wa ndani
na nje ya chama, aliyekuwa Mwenyekiti wa muda wa Mkutano Mkuu Maalum,
Mhe Julius Mtatiro alilazimika kuakhirisha Mkutano ule mara baada ya
kumalizika kwa ajenda ya kwanza ambapo Mkutano Mkuu uliridhia kujiuzulu
kwa Profesa Ibrahimu Haruna Lipumba kwa azimio lililoungwa mkono na
wajumbe 476 dhidi ya wajumbe 14 waliokataa. Hivyo basi agenda namba 2
haikuwahi kukamilishwa, na kwa hivyo haikufanyiwa maamuzi.
Kikao
cha Baraza Kuu la Uongozi, kilichokaa jana kimejadili kwa kina juu ya
hujuma za kuvuruga Mkutano Mkuu Maalum wa tarehe 21/08/2016.
Baraza
kuu limesikitishwa sana na kitendo kile ambacho mbali ya kukisababishia
chama hasara ya zaidi ya Shillingi milioni 600, pia kimepelekea
kuharibu taswira ya chama ndani na nje ya nchi.
Baraza
Kuu lilipata nafasi ya kupokea maelezo ya kina kutoka kwa wajumbe mbali
mbali hasa wale wanaotokea Tanzania Bara walioeleza kwamba hujuma
zilizofanywa kuvuruga Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa wa tarehe 21 Agosti,
2016 hazikuwa za bahati mbaya au za kushtukiza bali ni matokeo ya njama
na mbinu ovu na chafu ambazo zimekuwa zikipangwa na kutekelezwa chini
kwa chini kwa muda mrefu.
Wajumbe
wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa walieleza kwa ushahidi jinsi baadhi
ya viongozi wa Chama walioaminiwa na kupewa nyadhifa za juu walivyogeuka
na kuanza kutumiwa na maadui wa nje ya Chama kukihujumu Chama.
Baraza
Kuu limezingatia kuwa CUF ni chama cha kistaarabu, ni Chama cha
Kidemokrasia na ni Chama chenye kutoa matumini ya mabadiliko ya kweli
kwa Watanzania walio wengi. Vurugu zilizojitokeza ni aibu na fedheha kwa
chama chetu mbele ya macho ya Watanzania na wapenda demokrasia.
Baraza
Kuu la Uongozi la Taifa limeridhika kwamba watu hao waliokuwa vinara wa
vurugu na njama hizo ovu walipewa nafasi mara kadhaa kujirekebisha
dhidi ya mwendo wao huo dhidi ya Chama lakini waliendelea na vurugu na
hujuma zao hizo.
Kwa
hatua iliyofikia, Baraza Kuu limeona halina njia nyengine ya kukinusuru
Chama isipokuwa kuchukua hatua kali na madhubuti kukilinda Chama ambao
ni wajibu wake kikatiba.
Kwa
msingi huu basi, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kwa kauli moja
(unanimously) limeamua kuchukua hatua za kinidhamu kwa viongozi na
wanachama mbali mbali waliohusika kwa njia moja au nyengine katika
kuchochea vurugu zile.
Baraza
kuu limechukua hatua mbili kubwa ambazo ni kutoa karipio kali,
kusimamisha na kufukuza uanachama wahusika wote walioshiriki kuchochea
vurugu hizo.
Viongozi
waliopewa karipio kali kwa mujibu wa Katiba ya Chama, Ibara ya 83
(5)(b) ambao ni wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa ni:
1. Rukiya Kassim Ahmed
2. Athumani Henku
Viongozi
waliosimamishwa uanachama kwa mujibu wa Katiba ya Chama, Ibara ya 83
(5)(c), hadi hapo watakapopata fursa ya kujieleza mbele ya Baraza Kuu
ni;
1. Prof Ibrahim Haruna Lipumba
2. Magdalena Sakaya
3. Abdul Kambaya
4. Ashura Mustafa
5. Omar Mhina Masoud
6. Thomas Malima
7. Kapasha M. Kapasha
8. Maftaha Nachumu
9.Mohamed Habib Mnyaa
10. Haroub Shamis
11. Mussa Haji Kombo
Mwanachama
aliyefukuzwa chama ambaye alipata fursa ya kujieleza mbele ya Baraza
Kuu na kikao kuamua kumfukuza chama kwa mujibu wa Katiba ya Chama, Ibara
ya 83 (5)(c) ni aliyekuwa Kaimu Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Wazee wa
CUF (JUWACUF), Shashu Lugeye.
Kufuatia
maamuzi hayo, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limewateua viongozi mbali
mbali kukaimu nafasi mbali mbali zilizoachwa wazi.
Kwa
kuzingatia kwamba kutokamilika kwa Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa wa
tarehe 21 Agosti, 2016 kulipelekea kushindwa kufanyika kwa uchaguzi wa
Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Chama, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa
limetumia uwezo liliopewa na Katiba ya Chama, Ibara ya 101 na 118,
kuunda Kamati ya Uongozi ambayo itakuwa ikifanya kazi za Mwenyekiti na
Makamu Mwenyekiti hadi hapo uchaguzi wa kujaza nafasi hizo
utakapofanyika.
Baraza Kuu la Uongozi limewateua wafuatao kuwa wajumbe wa Kamati hiyo ya Uongozi:
1. Mhe. Julius Mtatiro – Mwenyekiti
2. Mhe. Katani Ahmed Katani – Mjumbe
3. Mhe. Severina Mwijage – Mjumbe
Aidha
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, kwa kufuata Ibara ya 105 (1) na (3) ya
Katiba ya Chama, limemteua Mhe. Joran Bashange kuwa Kaimu Naibu Katibu
Mkuu wa Chama kwa upande wa Tanzania Bara na Mhe. Mbarala Maharagande
kuwa Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma
hadi hapo nafasi hizo zitakapojazwa rasmi kwa mujibu wa masharti ya
Katiba ya Chama.
Mwisho,
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa linawahakikishia wanachama na wapenzi
wake na Watanzania wote kwa ujumla kuwa Chama Cha Wananchi – CUF kipo
imara na makini na katu hakitoyumbishwa kwa hila na njama ovu na chafu
zinazofanywa na maadui wa chama hichi. Tangu kuasisiwa kwake, CUF
imeandamwa na maadui wa kila aina, na imepitia katika misuko suko
mingi.
Tunaamini
hila na njama hizo ovu zimekuwa zikielekezwa CUF kwa kutambua kwamba
Chama hichi ndicho kinachobeba dhamira ya dhati ya kuleta mabadiliko ya
kweli hapa nchini.
Kutokana
na umadhubuti, umakini na uimara wa Katiba ya Chama na safu ya viongozi
wake, CUF imeweza kuvuka salama kila ilipoingia katika misuko suko hiyo
na kwa hivyo, hata wimbi hili lililoonekana kukitikisa Chama
limekabiliwa ipasavyo na sasa kazi iliyopo mbele yetu ni kuendeleza
harakati za kisiasa za kuwaletea Watanzania wa Bara na Zanzibar
mabadiliko wanayoyataka.
HAKI SAWA KWA WOTE
Nassor Ahmed Mazrui- +255 777 426 975
NAIBU KATIBU MKUU CUF
Mawasiliano: Mkurugenzi Habari - Salim Biman 077414112
K/Naibu Mkurugenzi : Mbarala Maharagande- 0784 001408
Imetolewa leo tarehe29/8/2016
No comments