Yanga yazima kelele za Azam
Haruna Niyonzima |
YANGA, jana
ilizidi kuziwashia taa ya kijani Simba na Azam FC, baada ya kutoka Uwanja wa
Taifa jijini Dar es Salaam kwa ushindi wa bao 1-0, bao lililofungwa na kiungo
wa kimataifa, Haruna Niyonzima katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Hiyo ni
ishara nzuri kwa wana Jangwani ambao msimu huu wamepania kuwapoka ubingwa
mahasimu wao wakubwa Simba, hasa baada ya kufanya maandalizi ya kutosha ya
kuweka kambi nchini Uturuki.
Matunda ya
kambi hiyo yameanza kuonekana, hasa baada ya mechi yake ya jana kuonesha soka
zuri la kuvutia mbele ya mashabiki wake waliofurika uwanjani hapo.
Yanga
walianza kwa kulisakama lango la Azam FC, ambapo dakika ya sita, Hamis Kiiza,
alipata nafasi nzuri na kupiga shuti kali lililodakwa na kipa Mwadin Ali.
Shambulizi
hilo liliwazindua Azam FC, dakika ya 10, Kipre Tchetche alijaribu kwa shuti
kali, lakini lilitoka nje, wakati tayari kipa wa Yanga, Ally Mustapha ‘Barthez’
akiwa tayari amepotea langoni kwake.
Dakika ya
16, Kiiza alimpasia pasi nzuri Jerryson Tegete akiwa amebaki na kipa, lakini
shuti lake kali lilitua mikononi mwa kipa Mwadin Ally.
Wakicheza
soka zuri la kuvutia, Yanga walipata nafasi nzuri na kulifikia lango la
wapinzani wao, lakini beki Joackim Atudo alifanya kazi nzuri ya kuokoa mpira
uliopigwa na Simon Msuva na kuwa kona tasa.
Dakika ya
32, Haruna Niyonzima, aliwainua vitini mashabiki wa Yanga baada ya kuifungia
timu yake bao zuri la kiufundi.
Tegete siku
ya jana haikuwa yake, kwani dakika ya 42 na 43, alishindwa kuipatia timu yake
mabao, badala yake akawa anaokoa, baada ya kushindwa kuunganisha mpira wavuni
uliopigwa na Haruna Niyonzima.
Yanga ambao
walitawala mchezo kipindi chote cha kwanza, kama wangekuwa makini wangeweza
kujipatia mabao zaidi ya matatu, lakini washambuliaji wake hawakuwa makini
kukwamisha mpira wavuni.
Kipindi cha
pili, Azam iliingia kwa lengo moja la kusaka bao la kusawazisha, dakika ya 65,
Barthez alifanya kazi ya ziada ya kupangua shuti kali lililopigwa na Kipre
Tchetche.
Wakiwa na
uchu za kusawazisha, Kipre Tchetche alipata nafasi nyingine dakika ya 72,
lakini shuti lake lilipanguliwa na kipa Barthez, mpira ambao ulitua miguuni kwa
Oscar Joshua na kuutoa na kuwa kona tasa.
Pamoja na
kipindi cha pili kubadilika na kuliandama lango la Yanga, lakini washambuliaji
wa Azam FC walikumbana na ukuta mgumu uliokuwa chini ya Kelvin Yondan na Nadir
Haroub ‘Cannavaro’, ambao walikuwa na kazi moja tu, ya kuondosha hatari langoni
kwao.
Kwa ushindi
huo, Yanga imezidi kuziwashia taa za kijani, Azam na Simba, ambazo ziko katika
nafasi ya kufukuzia ubingwa, ikiziacha kwa pointi tatu na nyingine pointi nane.
Baada ya
mchezo huo kumalizika, Mwamuzi Hashim Abdallah wa Dar es Salaam alisindikizwa
na askali waliokuwa wakilinda usalama uwanjani hapo, wakihofia kufanyiwa fujo
na mashabiki.
Yanga: Ally
Mustapha ‘Barthez’, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub Cannavaro, Kelvin
Yondan, Athuma Idd ‘Chuji’Simon Msuva, Frank Domayo, Jerryson Tegete/Didier
Kavumbagu, Hamis Kiiza/Said Bahanunzi, Haruna Niyonzima.
Azam FC: Ali
Mwadin, Kipre Balou/Jabir Aziz, Waziri Salum, Joackin Atudo, David Mwantika,
Ibrahim Mwaipopo, Abubakari Salum ‘Sure Boy’, John Bocco, Kipre Tchetche,
Hamphrey Mieno, Mcha Hamis.
No comments