Mbezi Veterans yaingia'mitini' kukwepa kipigo kutoka kwa Kijitonyama Veterans
Na Mwandishi Wetu
UONGOZI wa timu ya Kijitonyama Veterans umepitisha azimio la kutocheza mechi yoyote ya kirafiki dhidi ya timu ya Mbezi Veterans ya barabara ya Morogoro kutokana na kile ilichokiita ‘tabia si ya kiwanamichezo’.
Kauli hiyo ilitolewa na mratibu mkuu wa timu hiyo, Majuto Omary kufuatia kitendo cha timu hiyo kushindwa kutokea uwanjani katika mchezo wao maalum wa kirafiki uliopangwa kufanyika jana asubuhi kwenye uwanja wa Kijitonyama.
Majuto alisema kuwa mechi hiyo iliombwa na timu hiyo ya Mbezi na wao (Kijitonyama) kuwakubalia kutokana na ukweli kuwa michezo ni afya mbali ya kudumisha urafiki. Alisema kuwa mechi hiyo ilipangwa kuanza saa 2.00 asubuhi, na timu hiyo ilithibitisha nusu saa kabla ya mechi hiyo kuwa wanakuja na wapo katika maandalizi.
Alifafanua kuwa baada ya hapo, viongozi wa timu hiyo hawakuonekana uwanjani na mbaya zaidi hawakupokea simu zao walizokuwa wanapiga ili kujua wamefikia wapi. “Kinanchosikitisha ni kwamba, walituweka hapo uwanjani na mbali ya kuwatumia ujumbe wa simu ya mkononi kuwa wamefika wapi au wamekwama, hawakujibu chochote, hii inaonekana kuwa ni makusudi,” alisema Majuto.
Majuto ambaye pia ni kiongozi wa timu ya waandishi wa habari za michezo nchini (Taswa FC), alisema kuwa hiyo si mara ya kwanza kwa timu hiyo kushindwa kutokea uwanjani bila ya kutoa taarifa.
“Waliwahi kuomba kucheza na Taswa FC pale Leaders Club, tukawakubalia, lakini hawakutokea uwanjani na hata simu zetu wakawa hawapokei wala kujibu ujumbe kusema kuwa wameshindwa kuja, walituacha uwanjani na kupoteza muda, hii ni tabia yao,” alisema.
Alisema kuwa haya maamuzi ni ya kudumu na watajaribu kuzitahadharisha na timu nyingine kuhusiana na vitendo vya timu hiyo kwani ni vya kupotezea muda wanamichezo.
No comments