![]() |
Rais TFF, Leodegar Tenga |
Akizungumza
na Waandishi wa Habari katika ofisi za TFF jijini Dar es Salaam leo mchana
(Februari 19 mwaka huu), Rais wa TFF, Leodegar Tenga amesema FIFA imetuma barua
ikiagiza mchakato wa uchaguzi usimame baada ya kupata malalamiko.
Amesema
kutokana na mkanganyiko huo, FIFA katika barua yake ya leo (Februari 19 mwaka
huu- imeambatanishwa) imeagiza mkutano wa uchaguzi wa TFF ambao awali
ulipangwa kufanyika Februari 24 mwaka huu uahirishwe hadi hapo itakapotuma
ujumbe wake nchini.
Ujumbe
huo wa FIFA unatarajiwa kufika nchini katikati ya mwezi ujao (Machi) ambapo
utafanya tathimini ya hali hivyo, kutuma ripoti yake katika shirikisho hilo na
baadaye kutoa mwongozo wa nini kifanyike.
Rais
Tenga amewaomba radhi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kwa usumbufu uliojitokeza
kutokana na uamuzi huo wa FIFA, hivyo kwa sasa hakutakuwa tena na mkutano huo
mpaka hapo watakapopewa taarifa nyingi.
Amesema
TFF inakaribisha kwa mikono miwili uamuzi huo wa FIFA kwa sababu ni chombo
ambacho cha juu kimpira duniani, na hatua hiyo ina lengo la kuhakikisha kuwa kila
mhusika katika mchakato huo wa uchaguzi anapata haki yake.
“Nia
yetu ni kuona watu wanatendewa haki, na nia ya FIFA ni kutafuta ukweli. Hivyo
wahusika (waathirika) wajiandae, watumie wakati huu kuandaa hoja zao ili FIFA
wakifika wawasikilize, wapate maelezo ya kina kuhusu utaratibu na malalamiko
yaliyotolewa,” alisema Tenga.
Rais
Tenga amesema timu hiyo ya FIFA itakapofika yenyewe ndiyo itakayopanga
izungumze na nani kwa wakati gani, hivyo ni vizuri waathirika na vyombo vyote
vilivyohusika na mchakato wa uchaguzi wakajiandaa.
Amesema
ilikuwa ni muhimu suala hili likatatuliwa katika ngazi ya FIFA kwa lengo la
kuhakikisha uchaguzi utakapofanyika TFF inaendelea kuwa chombo kimoja badala ya
kurudi katika migogoro iliyokuwepo huko nyuma.
“Nataka
tubakie kama tulivyokuwa. Malumbano yaishe. Pangeni hoja, wakija hao
waheshimiwa (FIFA) muwaambie. FIFA ni chombo cha juu, nafurahi wamekubali
kuingia katika hili, kwani wana shughuli nyingi wangeweza kukataa,” amesema.
Kuhusu
fursa ya kufanya marejeo (review) kwenye Kamati ya Rufani ya Uchaguzi
inayoongozwa na Idd Mtiginjola ambayo aliielezea Jumamosi, Rais Tenga amesema
kwa vile hicho ndicho chombo cha mwisho nchini katika masuala ya uchaguzi
alishauriwa kuwa kingeweza kufanya review.
“Kwa
vile hakuna chombo kingine, nikashauriwa kuwa kinaweza kufanya review. Katika
utaratibu wa kutoa haki, uamuzi ni lazima uwe wa wazi kwa kutoa sababu.
Nilidhani hilo linawezekana, kwani Mahakama Kuu hufanya hivyo. Kwa hili uamuzi
wa Mtiginjola ni sahihi,” amesema Rais Tenga.
Kamati
ya Mtiginjola iliyokutana jana (Februari 18 mwaka huu) ilitupa maombi ya review
yaliyowasilishwa mbele yake na waombaji uongozi watano kwa vile hakuna
kipengele chochote kwenye Katiba ya TFF na Kanuni za Uchaguzi kinachotoa fursa
hiyo.
Waombaji
hao walikuwa Jamal Emil Malinzi aliyeenguliwa kugombea urais wa TFF na Hamad
Yahya aliyeondolewa kwenye kinyang’anyiro cha kuwania uenyekiti wa Bodi ya Ligi
Kuu (TPL Board).
Wengine
ni walioomba kuwania ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF na Kanda zao kwenye
mabano; Eliud Peter Mvella (Iringa na Mbeya), Farid Salim Nahdi (Morogoro na
Pwani) na Mbasha Matutu (Shinyanga na Simiyu).
No comments:
Post a Comment