Header Ads

ad

Breaking News

Azam yaichapa Al Nasri 3-1


 AZAM FC, jana walianza vizuri michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF), baada ya kuilaza Al Nasri ya Sudan Kusini mabao 3-1, katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Ukiwa ni mchezo wake wa kwanza wa kimataifa, ilifanikiwa kuibuka na ushindi huo nyumbani, hivyo kuwa na kibarua kigumu katika mchezo wa marudiano utakaochezwa wiki mbili zijazo nchini Sudan.
Washindi hao wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara, walikuwa wa kwanza kulifikia lango la wapinzani wao, lakini Kipre Tchetche alishindwa kufunga bao dakika ya 10, baada ya kupiga shuti kali lililopanguliwa na kipa Peter Midia.
Azam wakicheza kwa kujituma, walifanikiwa kupata bao la kwanza dakika ya 14, lililofungwa na Abdi Kassim ‘Babi’,  kwa kichwa akiunganisha mpira uliotoka kwa Hamphrey Mieno na kuujaza wavuni.
Dakika ya 21, Tchetche alipata nafasi nzuri ya kufunga, lakini alishindwa kuitimia vizuri krosi iliyotoka kwa Babi, baada ya shuti lake kupanguliwa na kipa wa Al Nasri.
Al Nasri wangeweza kusawazisha bao dakika ya 27, baada ya Kon James kuwatoka mabeki wa Azam na kupiga shuti kali lililodakwa na kipa Mwadin Ali.
Juhudi za Al Nasri zilizaa matunda dakika ya 39, baada ya Fabian Elius kuisawazishia bao timu yake, akitumia vizuri makosa ya mabeki wa Azam na kuujaza mpira kimiani.
Kipindi cha pili, Azam walipata nafasi nzuri ya kufunga bao, lakini Babi alishindwa kuwainua vitini mashabiki wao dakika ya 48, na mpira ukaondoshwa kwenye hatari na beki Joseph Odongi.
John Bocco aliyeingia kuchukua nafasi ya Babi, alishindwa kuitumia vizuri nafasi aliyopata dakika ya 68, baada ya mpira wa kichwa aliopiga kudakwa na kipa wa Al Nasri, Midia.
Kipre Tchetche, alifanya kazi nzuri na kuipatia timu yake ya Azam bao la pili dakika ya 80, kwa kichwa akiunganisha mpira wa krosi uliopigwa na Hamis Mcha na kujaa wavuni.
Dakika ya 84, Bocco alishindwa kuifungia timu yake bao baada ya shuti lake kali kupanguliwa na kipa Midia, kabla ya kumrudia, lakini shuti lake la mwisho mpira ukapaa juu ya lango la Al Nasri.
Kipre Tchetche aliwazidishia maumivu Al Nasri kwa kufunga bao la tatu dakika ya 90, akitumia vizuri pasi ya Mcha na kuukwamisha mpira wavuni.
Katika mechi hiyo, mashabiki wanaokaa jukwaa linaloaminika kutumiwa na Yanga, walikuwa wakiishangilia Al Nasri, hasa baada ya kuwaona wakiwa katika jezi zenye rangi ya njano.
Lakini, ushindi huo wa Azam, unaweza kuwa salama tosha kwa Yanga, ambao watavaana wiki ijayo katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Azam: Mwadini Ally, Himid Mao, Malika Ndeule, David Mwantika, Jockins Atudo, Michael Bolou, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Humphrey Mieno, Brian Umony, Abdi Kassim ‘Babi’/John Bocco na Tchetche Kipre.
Al Nasr: Peter Midia, Joseph Odongi, Mskin Ammanuel, Abdallah Sebit,  Simon Amanya, Johnson James, Abdallmelik Sebit, Ladu Manas, Kon James, Jacob Osuru, Fabian Elias.

No comments