Yondani, Twite, Akuffo, Ochieng kwa raha zao
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Septemba 11, 2012
Kamati
ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) ilikutana jana (Septemba 10 mwaka huu) ili kupitia na kutoa
uamuzi/ushauri kwa masuala mbalimbali yaliyowasilishwa mbele yake.
Wajumbe
sita kati ya saba waliopo walihudhuria kikao hicho chini ya Mwenyekiti Alex
Mgongolwa. Wajumbe hao ni Hussein Mwamba, Imani Madega, Ismail Aden Rage, Llyod
Nchunga na Omari Gumbo.
Suala
la ugombea wa Michael Wambura katika FAM
Michael
Wambura aliomba uongozi katika Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mara (FAM)
katika uchaguzi uliofanyika Novemba mwaka jana. Kamati ya Uchaguzi ya TFF
iliondoa jina lake kwa kukosa sifa ya kugombea nafasi hiyo.
Wambura
hakuridhika na uamuzi huo akapeleka shauri lake Kamati ya Nidhamu ya TFF.
Kamati hiyo katika uamuzi wake ilisema haina mamlaka ya kushughulikia shauri
hilo. Baadaye Wambura alikata rufani katika Kamati ya Rufani ya TFF ambayo
ilimpa haki ya kugombea.
Kutokana
na mkanganyiko huo wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF kuwa na uamuzi wa mwisho katika
masuala ya uchaguzi ya wanachama wa TFF, na uamuzi wa Kamati ya Rufani kuhusu
uchaguzi wa mwanachama wa TFF, Sekretarieti ya TFF iliomba mwongozo wa kisheria
kwa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji.
Kwa
vile Kamati hizo mbili (Uchaguzi na Rufani) haziko katika mtiririko wa moja kwa
moja wa utoaji maamuzi, Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji
iliishauri Sekretarieti ya TFF kuliandikia Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa
Miguu (FIFA) ili kupata muongozo juu ya suala hilo.
Katika
muongozo wake, FIFA ilitoa maoni kuwa kwa mujibu wa Katiba ya TFF chombo cha
mwisho cha rufani katika masuala ya uchaguzi kwa wanachama wa TFF ni Kamati ya
Uchaguzi ya TFF. Hata hivyo, FIFA ilishauri kuwa si vizuri chombo kimoja kikawa
msimamizi wa uchaguzi, na chenyewe tena ndiyo kiwe cha mwisho katika uamuzi
kwenye uchaguzi husika.
Hivyo,
Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji imetoa mapendekezo mawili
kwenda Kamati ya Utendaji kwa ajili ya marekebisho ya Katiba ili kiwepo chombo
kingine cha rufani pale mgombea anapopinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF.
Mapendekezo
hayo ni; Iundwe Kamati ambayo itakuwa inasikiliza rufani zote zinazotokana na
uamuzi uliofanywa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF, hivyo Kamati ya Uchaguzi ya TFF
isiwe chombo cha mwisho cha uamuzi kwa rufani zinazotokana na uchaguzi wa
wanachama wa TFF.
AU. Rufani zote
zinazotokana na uchaguzi wa wanachama wa TFF zisikilizwe na Kamati ya Rufani ya
TFF. Kwa maana hiyo Kamati ya Rufani ya TFF ndiyo kiwe chombo cha mwisho kwa
wasiokubaliana na uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF kuwasilisha malalamiko yao.
USAJILI/PINGAMIZI
DHIDI YA WACHEZAJI
Musa
Hassan Mgosi, Ayoub Hassan Isiko
Mchezaji
Musa Hassan Mgosi ameombewa usajili Ruvu JKT kutoka DC Motema Pembe ya Jamhuri
ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), na Ayoub Hassan Isiko ameombewa usajili Mtibwa
Sugar kutoka Bull FC ya Uganda. Wachezaji hao hawaruhusiwi kuchezea timu hizo
mpaka Hati zao za Uhamisho wa Kimataifa (ITC) zitakapokuwa zimepatikana.
Toto
dhidi ya Kagera Sugar kumsaini Enyinna Darlinton Ariwodo
Toto
Africans ilipinga usajili wa Enyinna Darlinton kwa timu ya Kagera Sugar kwa
vile bado ina mkataba wa mchezaji huyo ambao unamalizika mwakani.
Kwa
upande wake Kagera Sugar ilisema imemsaini mchezaji huyo kwa vile Toto Africans
imeshindwa kumlipa mshahara ambapo kuna makubaliano rasmi kati ya Ariwodo kuwa
klabu hiyo ikishindwa kumlipa mshahara anaruhusiwa kuondoka.
Uamuzi
wa Kamati ni kuwa Ariwodo ni mchezaji halali wa Kagera Sugar kwa vile Toto
Africans ilishindwa kutimiza masharti ya mkataba.
Ramadhan
Chombo ‘Redondo’
Redondo
ameidhinishwa kuchezea Simba kwa kuzingatia mchezo wa haki na uungwana (Fair
Play) baada ya klabu hiyo na ile ya Azam kufikia makubaliano kuhusu mchezaji
huyo.
Mchezaji
David Luhende kusajiliwa Yanga
Yanga
ilikiri kutolipa ada ya uhamisho ya sh. milioni 5 kama walivyokubaliana na
Kagera Sugar. Awali waliipa Kagera Sugar hundi iliyogonga mwamba benki (bounced
cheque). Shauri hilo lilimalizwa kwa Yanga imetakiwa kulipa fedha hizo ndani ya
siku 21 kuanzia Septemba 10 mwaka huu.
Super
Falcon dhidi ya Edward Christopher kusaini Simba
Simba
imepewa siku 21 kuanzia Septemba 10 mwaka huu iwe imeilipa Super Falcon fedha
za matunzo (compensation) kwa vile ndiyo iliyomlea mchezaji Edward Christopher
aliyesajiliwa katika klabu hiyo.
Toto
Africans dhidi ya Mohamed Soud kusajiliwa Coastal Union
Toto
Africans iliweka pingamizi kwa maelezo kuwa bado ina mkataba na mchezaji huyo.
Hivyo kwa msingi wa Fair Play, mchezaji huyo ameidhinishwa Coastal Union baada
ya makubaliono kati ya klabu.
Rollingstone
dhidi ya Kigi Makassy kusajiliwa Simba
Simba
imetakiwa kuilipa Rollingstone gharama za matunzo ilizoingia wakati ikiwa na
mchezaji huyo kwa kuzingatia kanuni za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa
Miguu (FIFA).
Super
Falcon dhidi ya Sultan Juma Shija kusajiliwa Coastal Union
Uamuzi
wa Kamati ni kuwa Shija atachezea Coastal Union, na kwa vile yuko chini ya umri
wa miaka 23, Coastal Union itailipa Super Falcon fidia ya fedha ilizotumia
kumhudumia mchezaji huyo.
African
Lyon dhidi ya Razak Khalfan kusaini Coastal
Lyon
imesema bado ina mkataba na mchezaji huyo. Kamati imebaini kuwa mkataba wa
mchezaji huyo na Lyon umemalizika, hivyo ni mchezaji halali wa Coastal Union.
Flamingo
dhidi ya Kelvin Friday kusajiliwa Azam
Friday
ruksa kucheza Azam, lakini klabu hiyo imepewa siku 21 kuanzia Septemba 10 mwaka
huu kuilipa Flamingo gharama za kuvunja mkataba.
Super
Falcon dhidi ya Robert Joseph Mkhotya kusaini African Lyon
Lyon
imeagizwa kuilipa Super Falcon sh. milioni moja ikiwa ni fidia ya kuvunja
mkataba wa mchezaji huyo ambaye imemsajili. Fedha hizo zitalipwa kwa awamu nne
kutokana na makato ya mlango yatakayofanywa na TFF. Falcon itapokea malipo hayo
kupitia TFF.
Oljoro
JKT dhidi ya Othman Hassan kusajiliwa Coastal
Kwa
mujibu wa rekodi za TFF, mkataba wa mchezaji huyo na Oljoro JKT unamalizika
mwakani. Hivyo, Othman Hassan ni mchezaji halali wa Oljoro JKT kwa vile bado
ana mkataba na klabu hiyo.
Yanga
dhidi ya Simba kuacha wachezaji wanne
Kamati
imetupa pingamizi hizo kwa vile hakuna malalamiko yoyote kutoka kwa wachezaji
juu ya kuvunjiwa mikataba yao. Wachezaji hao walioachwa na Simba ni Dan
Mrwanda, Haruna Shamte, Kanu Mbiavanga na Lino Masombo.
Ikiwa
wachezaji hao watakuwa na malalamiko kuhusu kuvunjiwa mikataba suala hilo
litafikishwa katika Kamati kwa ajili ya kusikilizwa na kutolewa uamuzi.
Mbuyu
Twite
Kwa
mujibu wa Ibara ya 18(3) ya Kanuni za Hadhi na Uhamisho wa Wachezaji wa
Kimataifa za FIFA, Yanga ilifuata taratibu zote katika kumsajili Mbuyu Twite,
hivyo ni mchezaji wake halali. Hata hivyo, kwa vile Yanga imekiri kuwa mchezaji
huyo alichukua dola 32,000 za Simba na kukiri kuzirejesha, kwa msingi wa kanuni
ya Fair Play, Kamati imeipa Yanga siku 21 iwe imelipa fedha hizo Simba.
Kelvin
Yondani
Kwa
mujibu wa Ibara ya 44(3) ya Kanuni za Uhamisho wa Wachezaji za TFF, Yanga
ilifuata taratibu zote katika kumsajili Kelvin Yondani, hivyo ni mchezaji wake
halali.
Kwa
vile Simba imesema mchezaji huyo vilevile alisaini mkataba na klabu yao,
imetakiwa kupitia mamlaka nyingine kuthibitisha hilo, na baada ya uthibitisho
iwasilishe malalamiko yake kwenye Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za
Wachezaji, au mamlaka zozote za kisheria kwa mujibu wa madai/lalamiko husika.
Alex
Mgongolwa
Mwenyekiti
Kamati
ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji
No comments