Nani kubeba ubingwa wa Bara msimu huu?
LIGI Kuu Tanzania Bara msimu wa mwaka 2011/2012 unanza
kutimua vumbo leo, ambapo jumla ya vilabu 14 vitaumana katika mechi za fungua
dimba.
SIMBA
Mabingwa watetezi wa ligi hiyo Simba, watakuwa Uwanja wa
Taifa jijini Dar es Salaam, kufungua dimba dhidi ya African Lyon pia ya jiji
hilo.
Simba ambao Jumanne ya wiki hii waliichapa Azam FC mabao
3-2 na kunyakua Ngao ya Jamii, wanapewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwenye
msimu mpya wa ligi hiyo, ingawa wanaonekana kuwa na udhaifu katika safu ya
ulinzi na kiungo mkabaji.
Pamoja na hilo, lakini timu hiyo inaonekana kuwa na
makali ya kutisha kwenye idara ya ushambuliaji.
Kwenye safu hiyo ya ushambuliaji, kuanzia viungo wa kati
na pembeni, kuna wachezaji wakali kama Mrisho Ngassa, Emmanuel Okwi, Danniel
Akuffo, Abdallah Juma, Felix Sunzu na Haruna Moshi ‘Boban’.
Kikosi hicho ambacho kinanolewa na kocha kutoka Serbia
Milovan Cirkovic, kimechukua taji hilo la Tanzania Bara mara 18.
Yanga
Mahasimu wakubwa wa Simba, Yanga, ambao wanashikilia
rekodi ya kuchukua ubingwa wa ligi hiyo mara 22, nao wanapewa nafasi kubwa ya
kutwaa ubingwa kuliko hata mahasimu wao hao.
Hiyo ni kutokana na usajili mzuri waliofanya msimu huu,
tena kwa kuchukua vijana wengi wazuri kutoka hapa nchini.
Na hata usajili wao kwa upande wa wachezaji wa kigeni,
imekuwa ni tofauti na miaka iliyopita, kwani miaka ya nyuma walikuwa wakinunua
wachezaji kwa gharama kubwa tofauti na viwango vyao.
Mmoja wa wachezaji wa kigeni ambao walinunuliwa na Yanga
misimu iliyopita, huku wakiwa na viwango vibovu ni Jama Mba Robert kutoka
Cameroon.
Kwa sasa Yanga imesajiliwa ‘mawe’ ya ukweli kutoka
ugenini, ambao ni Mbuyu Twite wa FC Lupopo ya DR Congo, Didier Kavumbangu
kutoka Atletico ya Burundi, huku ikiwa na wageni wengine hatari kama Haruna
Niyonzima (Rwanda) na Hamisi Kiiza (Uganda).
Kwa upande wa wachezaji wa nyumbani, wamewasajili akina
Said Bahanunzi kutoka Mtibwa Sugar, Ally Mustafa ‘Barthez’ (Simba), Juma Abdul,
David Luhende (Kagera) Sugar, Kelvin Yondan (Simba), Frank Domayo (Ruvu
Shooting), Simon Msuva na Nizar Khalfan.
Kwa wachezaji hao ukichanganya na wale wa zamani kama
akina Athumani Iddi ‘Chuji’, Juma Seif ‘Kijiko’, Shamte Ally, Jerryson Tegete,
Job Ibrahim, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Rashid Gumbo na Nurdin Bakari, ni wazi
Yanga wataleta ushindani mkubwa kama si kuipora Simba ubingwa, baada ya msimu
uliopita kushika nafasi ya tatu.
AZAM FC
Azam hawajafanya usajili wa kutisha kwenye kikosi chao
msimu huu zaidi ya kumwongeza mlinda mlango Deogratias Munishi ‘Dida” kutokana
Mtibwa Sugar ili kusaidiana na kipa mwingine Mwadini Ally.
Kikosi hicho cha Azam, kama kitakuwa makini, nacho
kinaweza kunyakua ubingwa wa ligi hiyo, kwa kuwa ni kikosi kizuri ambacho
kimeonesha upinzani mkubwa msimu uliopita na kushika nafasi ya pili.
Klabu hiyo yenye makazi yake Chamazi, nje kidogo ya Jiji
la Dar es Salaam, pamoja na kuwa na miaka sita tu kwenye ligi hiyo, imeonekana
kuwa kivutio na washindani wa kweli kwenye ligi hiyo.
Kwa kutokufanya usajili, hakuwafanyi kukosa nafasi ya
kutwaa ubingwa, kwa kuwa bado wana kikosi kizuri kinachotandaza soka safi.
Azam wanawategemea zaidi washambuliaji wao John Bocco na
Kipre Tchetche raia wa Ivory Coast, ambao wamekuwa mwiba mchungu kwa timu
pinzani katika mechi kadha wa kadha.
Katika kiungo, kuna vipaji kama Abdi Kassim ‘Babi’,
Ibrahim Mwaipopo, Abdulrahim Humoud, Salum Abubakari (Sure Boy Jr), Himid Mau
na wengineo.
Pamoja na wachezaji hao, Azam ina ukuta mzuri unaoundwa
na kuongozwa na nahodha Aggrey Morris, Said Morad na Erasto Nyoni ambaye kwa
sasa kiwango chake ni cha juu mno.
Mtibwa SUGAR
Tangu mwaka 2000 Mtibwa wachukue taji la ligi hiyo,
haijaonyesha makali yake, lakini wamekuwa wakitoa upinzani mkubwa kila msimu.
Nafasi ya kikosi hicho cha Mtibwa kutwaa ubingwa si kubwa
sana, ingawa wanatarajiwa kutoa upinzani kama misimu mingine iliyopita.
Mtibwa wamemuongeza mchezaji aliyewahi kuichezea klabu
hiyo zamani, Shaaban Kisiga na kumrejesha Shaaban Kado aliyekuwa Yanga, ambao
wataungana na wachezaji wengine kama Shaaban Nditi na Hussein Javu kuhakikisha
wanafanya vizuri msimu huu.
COASTAL UNION
Ukiachana na Mtibwa, timu ya Coastal Union ‘Wagosi
Wakaya’ ya Tanga, nayo inatarajiwa kuleta upinzani mkubwa kutokana na jinsi
walivyojipanga, baada ya kuonyesha cheche zao mzunguko wa pili msimu uliopita.
Klabu hiyo ilivurunda vibaya katika msimu wa kwanza wa
ligi hiyo na kupokea vipigo vya mbwa mwizi kama kile cha mabao 5-0 dhidi ya
Yanga.
Lakini mzunguko wa pili, mabingwa hao wa mwaka 1988,
walibadilika na kutoa vipigo na kuwafanya kushika ya tano kwenye ligi hiyo.
Klabu hiyo yenye maskani yake Barabara ya 11 mjini Tanga,
inapewa nafasi kubwa ya kuleta upinzani kwenye kinyang'anyiro cha kuwania taji
hilo la Tanzania Bara.
Kikosi chao kimefanya usajili 'bab kubwa' kwa kuwasainisha
nyota kama Mkenya Jerry Santo, Razak Khalifan, Kassim Seleman ‘Selembe’, Nsa
Job, Green Atupile na Juma Jabu aliyetokea Simba.
Kagera Sugar
Kagera Sugar nayo ni moja ya timu zinazotoa upinzani
mkuwa kwenye ligi hiyo, huku ikiwa na kikosi kilichomudu kubaki kwenye kiwango
kizuri ingawa hakijawahi kuchukua ubingwa.
Timu hiyo yenye yenye makazi yake kwenye mashamba ya miwa
ya Kagera, msimu huu imewasajili wachezaji kama Enyinna Darlinton na Benjamin
Ese Fuyo wote kutoka Nigeria, Salum Kanone (Moro United), Malika Ndeule na
Zuberi Dabi (Villa Squad).
JKT RUVU, JKT OLJORO
NA RUVU SHOOTING
JKT Ruvu, Ruvu Shooting na JKT Oljoro ni timu ambazo
zilionesha soka safi, japokuwa hazikuweza kufanikiwa kufanya mambo makubwa
katika msimu uliopita.
JKT Ruvu wamemsajili Credo Mwaipopo na Mussa Hassan
‘Mgosi’, jambo linalowapa matumaini ya kuweza kufanya vizuri kwenye ligi hiyo,
ingawa si kuchukua ubingwa.
Kwa upande wa Ruvu Shooting watakuwa na wakati mgumu
kuweza kukaa sawa kwenye msimu huu wa ligi, baada ya kuwauza wachezaji wake
muhimu.
Ruvu imemuuza Abdallah Juma na Paul Ngalema kwenda Simba,
huku kiungo Frank Damayo akitua Yanga.
Oljoro wameweza kubaki kwenye kwenye ligi hiyo, baada ya
kupanda msimu uliopita, huku wakionesha soka safi ingawa nao hawana nafasi ya
kutwaaa upingwa.
African Lyon
African Lyon si timu ya kuchukua ubingwa nah ii inatokana
na madai ya uongozi wa klabu hiyo, kuwa wao wako kwenye ligi kuu ya bara kwa
ajili ya kuinua vipaji.
Toto African
Hali hiyo ipo pia kwa Toto African, ambao nao wamekuwa wakijiandaa
msimu mzima kwenye ligi kwa ajili ya kuifunga Simba na si kuleta ushindani
wowote kwenye ligi.
Polisi Moro, Prisons NA JKT
Mgambo
Timu zilizobaki ni zile zilizopanda daraja msimu huu,
ambazo ni Polisi Moro, Prisons ya Mbeya na JKT Mgambo ya Tanga.
Kwa klabu hizo kwa sasa zitakuwa zikifikiria kubaki
kwenye ligi hiyo kwanza na si kufikiria kuchukua nafasi ya juu.
Kwa upande wake, Prisons huenda ikawa tofauti kwa kuwa ni
timu yenye uzoefu mkubwa na ligi hiyo, hivyo inaweza ikatoa upinzani kwa vigogo
wa ligi hiyo.
No comments