APRM yamlilia Meles Zenawi
![]() |
Marehemu Meles Zenawi (kushoto) wa Ethiopia na Hu Jintao wa China |
Na Hassan Abbas
Mpango wa Afrika
Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) umeungana na viongozi wa Bara la Afrika,
wananchi wa Ethiopia na wabia wengine wa maendeleo ya Afrika kuomboleza kifo
cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia, Meles Zenawi.
Kwa mujibu wa taarifa
iliyotolewa na uongozi wa APRM makao makuu nchini Afrika Kusini na nakala yake
kupatikana jijini Dar es Salaam jana, uongozi wa taasisi hiyo ambayo Zenawi
alikuwa ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Marais inayosimamia APRM, umeeleza kuwa kifo
cha Zenawi kimeacha simanzi kuu na pengo katika uongozi wa mchakato huo.
“Jopo la Watu Mashuhuri
la APRM limepokea kwa masikitiko na mstuko mkuu kifo cha Melesi Zenawi, Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Ethiopia aliyekuwa pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Marais na
Viongozi wa Afrika wanaoiendesha APRM.
“Kwa niaba ya Jopo hili
na Sekretarieti ya APRM makao makuu, na kwa niaba yangu binafsi, tunapenda
kuwasilisha salamu za pole za familia ya APRM barani Afrika kwa Serikali na watu
wa Ethiopia,” ilisema taarifa hiyo iliyosainiwa na Mwenyekiti wa Jopo hilo,
Prof. Amos Sawyer, Rais wa zamani wa Serikali ya mpito ya Liberia.
Kwa mujibu wa taarifa
hiyo, APRM imemueleza Zenawi, aliyekuwa kiongozi wa Kamati hiyo ya Marais tangu
mwaka 2007 kuwa amechangia kwa kiasi kikubwa kuisukuma mbele taasisi hiyo ya
kutathmini utawala bora barani Afrika ikiwa ni mapenzi yake kwa maendeleo ya
watu wa Afrika.
“Kifo chake kimeacha
huzuni na mstuko barani Afrika hasa wakati huu ambapo ameiacha APRM ikiwa
taasisi inayokua kimajukumu na kiuongozi,” alisema Prof. Sawyer.
Akiwafariji wafiwa,
Prof. Sawyer alisema Zenawi atakumbukwa kwa mema aliyoyafanya. “Katikati ya
maombolezo haya, tunaamini familia yake na wadau wa APRM watafarijika na jambo
moja kuu-mambo mema aliyoyatenda Zenawi wakati wa uhai wake,” imehitimisha
taarifa hiyo.
APRM ni mchakato
uliobuniwa na viongozi wa Bara la Afrika mwaka 2003 kwa nia ya kutathmini
utawala bora katika kila nchi mwanachama kwa lengo la Afrika kujikosoa na
kujisahihisha ili kuwaletea watu wake maendeleo.
Tanzania ni miongoni
mwa nchi 34 kati ya 54 za Afrika zilizokwishajiunga moaka sasa na mchakato wa
APRM na iko katika maandalizi ya kuwasilisha ripoti yake ya hali ya utawala
bora kwenye kikao cha wakuu wa nchi za APRM cha Januari mwakani ili ijadiliwe
na kupewa maoni ya kufanyiwa kazi.
Tayari Serikali ya
Tanzania kupitia taarifa ya Rais Jakaya Kikwete imekwishatoa rambirabi kufuatia
kifo hicho cha Zenawi aliyekuwa pia akiongoza programu kadhaa za Umoja wa
Afrika ikiwemo NEPAD.
No comments