TFF YAMPONGEZA MAKUNGU KUCHAGULIWA MWENYEKITI MPYA WA ZFA
Shirikisho la Mpira
wa Miguu Tanzania (TFF) linampongeza Amani Ibrahim Makungu kwa kuchaguliwa kuwa
Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) katika uchaguzi uliofanyika
juzi (Juni 30 mwaka huu) kwenye hoteli ya Bwawani, mjini Zanzibar.
Ushindi wa asilimia
94 alioupata Makungu ambaye hakuwa na mpinzani katika uchaguzi huo mdogo
unaonesha imani ambayo wajumbe wa Mkutano Mkuu wa ZFA wanayo kwake katika
kukiongoza chama hicho.
Ni matarajio ya TFF
kuwa ushindi huo utatafsiriwa kwa vitendo na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa ZFA na
wadau wa mpira wa miguu Zanzibar kwa kumpa Makungu ushirikiano wa asilimia 100
ili kuhakikisha Kamati yake ya utendaji inafanya kile kinachotarajiwa na wengi.
Makungu si mgeni
katika mpira wa miguu, na mchango aliotoa kwa mchezo huo visiwani kabla ya
kuwania nafasi hiyo unatambuliwa na kila anayefuatilia maendeleo ya mpira wa
miguu katika Zanzibar.
TFF tunaahidi
kuendelea kutoa ushirikiano kwa ZFA chini ya Makungu kama ilivyokuwa kwa
mtangulizi wake Ali Ferej Tamim ili kuhakikisha ustawi wa mpira wa miguu
visiwani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
No comments