Header Ads

ad

Breaking News

Simba, Azam fainali ya Ujirani Uwanja wa Taifa kesho


Simba SC
MABINGWA wa soka wa  Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, na mabingwa wa Kombe la Mapinduzi Zanzibar, Azam FC, kesho zitashuka Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kuumana katika mechi ya fainali ya Kombe la Ujirani Mwema.

Awali, michuano hiyo ilikuwa ikichezwa kisiwani Zanzibar, lakini hatua ya fainali imehamishiwa jijini Dar es Salaam. 

Uamuzi huo umefikiwa jana baada ya timu hizo mbili kujadiliana na uongozi wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) na kuamua kuihamishia  Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kuisongeza mbele siku moja.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zilisema kwamba, Simba na Azam ziligoma kuendelea kuutumia Uwanja wa Amani mjini humo, kwa madai kuwa, ni mbovu.

“Timu hizi zilikuwa zikitumia uwanja huu huku zikilalamika kuwa, ni mbovu na wachezaji wao wameumia,” kilisema chanzo hicho.

Habari zaidi zilisema kuwa, Simba na Azam, zote zina wachezaji watatu waliokuwa majeruhi, ambao waliumia wakati wakizichezea timu zao kwenye Uwanja huo wa Amani.

Kutokana na ubovu huo, viongozi wa timu hizo ambazo zitashiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), waliamua kuhamishia mechi hizo kwenye uwanja ambao utawafanya wachezaji wao wachezaji bila ya hofu.

Chanzo hicho kiliongeza kwamba, Kampuni ya Prime Time Promotion, ndio waliochukua pambano hilo na watatoa sh. milioni 25 kwa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), mshindi sh. milioni 10 na wa p[ili sh. milioni tano.  

Awali, fainali hiyo ilikuwa ichezwe leo kwenye Uwanja wa Amani Zanzibar, lakini baada ya kuihamishia jijini Dar es Salaam, wameamua kusogeza mbele siku moja.

Mara ya mwisho timu hizo zilikutana katika hatua ya makundi na kutoka sare ya bao 1-1, mabao hayo yalifungwa na wachezaji wapya wa timu hizo waliosajiliwa kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu, Dany Mrwanda kwa upande wa Simba na Azam FC ikasawazaisha kupitia kwa George Odhiambo ‘Blackberry’.

Pamoja na kutoka sare katika mchezo huo, Azam FC walicheza pungufu baada ya kiungo wake, Abdulhalim Humoud, kutolewa nje kwa kadi kuoneshwa kadi nyekundu dakika ya 52,  baada ya kuoneshwa kadi ya njano mara mbili kwa kucheza vibaya.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa mkali na wa kusisimuwa, kutokana na timu hizo kuwa na upinzani wa hali ya juu, huku kila moja iktumia wachezaji wapya waliosajiliwa kwa ajili ya ligi ya Bara msimu ujao.
Azam FC

No comments