Yanga yatuma salamu timu zitakazoshiriki Kagame
![]() |
Yanga |
MABINGWA
wa soka Afrika Mashariki na Kati, Yanga, wametuma salamu kwa timu
zitakazoshiriki michuano ya Kombe la Kagame baada ya jana kuichezesha samba la
Kispania, JKT Ruvu katika mchezo wa kirafiki uliofanyika kwenye Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam.
Katika
mchezo huo, Yanga ilishinda mabao 2-0 yaliyofungwa na beki Nadir Haroub
‘Cannavaro’ na mshambuliaji Hamis Kiiza akitokea benchi.
Mbali ya
ushindi huo, kiwango kilichoonyeshwa na Yanga jana ndicho hasa kilichowachengua
mashabiki wake ambao muda wote wa mchezo huo dhidi JKT Ruvu wanaosifika kwa
soka la kitabuni, walikuwa wakishangilia soka iliyoonyeshwa na vijana wao hao.
Na kwa
kuwa wakongwe hao wa soka nchini walikuwa wakicheza na timu inayojua kusakata
kandanda hasa, haikuwa shida kwa vijana wa Jangwani kuonyesha uwezo wao
uwanjani hapo.
Japo
timu hiyo imeanza kambi hivi karibuni tofauti na JKT Ruvu ambao huwa wapo
kambini kwa muda mrefu, vijana wa Jangwani hawakupata shida dhidi ya wapinzani
wao kuonyesha nini wamevuna ndani ya muda huo mfupi, chini ya Kocha Mkuu
Mbelgiji Tom Saintfiet na msaidizi wake, Fred Felix Minziro.
Miongoni
mwa wachezaji waliong’ara jana ni kiungo Mnyarwanda Haruna Niyonzima, Kiiza,
Rashid Gumbo, Nizar Khalfan, beki mpya wa pembeni David Luhende, Kelvin Yondani
aliyejiunga na timu hiyo akitokea Simba, Juma Abdul, Jerry Tegete na
wengineo.
Kati ya
wote hao, Niyonzima ndiye aliyechengua zaidi uwanjani hapo kutokana na ufundi
wake katika kuchezea mpira, pasi ‘zilizokwenda shule’, na zaidi ikiwa ni uwezo
wake wa kutumia akili awapo na mpira.
Kwa
kiasi kikubwa, Niyonzima ndiye aliyekuwa nyota wa mchezo wa jana, huku
akifuatiwa na Luhende ambaye alionyesha kiwango cha hali ya juu katika nafasi
aliyocheza ya beki wa kushoto, zaidi ikiwa ni katika kupiga krosi kwa ufundi wa
hali ya juu.
Niyonzima
alikuwa akiwasunguka kama alivyotaka wachezaji
wa JKT Ruvu, ikiwa ni pamoja na kupiga krosi iliyozaa bao la pili lililofungwa
na Kiiza kwa kifua na hivyo kuwapagawisha wapenzi wa timu hiyo.
Kwa
upande wake, Gumbo ambaye alikuwa akisotea benchi enzi za Kocha Kostadin Papic,
jana aliwaonyesha wapenzi wa timu hiyo kile walichokuwa wakikikosa kutoka kwake
kutokana na jinsi alivyokuwa akitamba katika eneo la kiungo akishirikiana na
Niyonzima, Nizar, Athuman Idd ‘Chuji, Tegete, Said Bahanuzi na wengineo.
Kwa
ujumla, Yanga jana walionyesha dalili nzuri ya kufanya vyema katika michuano ya
Kombe la Kagame kutokana na uchezaji wao kupitia mfumo wa 3:5:2 na wakati
mwingine 3:5:1:1.
No comments