NAMNA DOKTA ULIMBOKA ALIVYOKAMATWA NA KUTESWA KINYAMA.
Dr. Ulimboka's saga....In his own words?
NAMNA DOKTA ULIMBOKA ALIVYOKAMATWA NA KUTESWA KINYAMA.
"NI saa 12:45 asubuhi, bado kiza kimetanda katika eneo hili la Msitu wa
Mabwepande. Mbele yangu namwona mtu akiwa amekaa chini, pembeni ya
barabara akiwa amelowa damu mwili mzima.
"Ninapomkaribia
nasikia sauti ya mtu huyo ikisema kwa taabu; naomba msaada jamani…
naomba msaada jamani, hivi ndivyo anavyoanza kusimulia Juma Mgaza
Abdallah, mtu wa kwanza kumwona Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari
Tanzania, Dk Steven Ulimboka baada ya kutekwa, kupigwa na kutupwa katika
Msitu wa Mabwepande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Abdallah, anasema mara baada kumwona daktari huyo akiwa katika hali
hiyo, alijaribu kumkokota kumtoa eneo hilo, lakini alishindwa kutokana
na hali mbaya aliyokuwa nayo.
Baada ya hapo, aliamua kusubiri mtu mwingine apite eneo hilo ili amwombe wasaidiane kumpeleka Kituo cha Polisi Bunju.
Anasema muda mfupi baadaye aliona gari likija mbele yao, akalinyooshea
mkono kulisimamisha. Liliposimama, akamweleza dereva hali aliyokuwa nayo
Dk Ulimboka na kwamba anahitaji msaada wa haraka.
Abdallah
ambaye hadi wakati huo alikuwa hamfahamu mtu ambaye alikuwa akimsadia
kuwa ni kiongozi wa madaktari kutokana na sura yake kuvimba, anasema
walimwingiza katika gari hilo na kumpeleka Kituo Kidogo cha Polisi
Bunju.
Anasema, Dk Ulimboka wakati huo alikuwa akiendelea
kuvuja damu katika baadhi ya majeraha yake huku akiwa hana suruali na
kubaki na bukta tu, huku akizungumza kwa taabu.
Kituo cha Polisi Bunju
Baada ya kumfikisha kituoni hapo, walitoa maelezo namna walivyomwokota na kumsaidia kumfikisha hapo.
Polisi baada kumhoji Dk Ulimboka, aliwatajia namba ya simu ya rafiki
yake aitwaye Dk Deo. Walipompigia na kumweleza tatizo hilo, aliamua moja
kwa moja kwenda Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, kutoa taarifa
hizo na hatimaye kuandamana na watu kadhaa kutoka hapo akiwamo
Mkurugenzi wake, Hellen-Kijo Bisimba.
Wawasili kituoni
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania wa kituo
hicho, Onesmo Olengurumwa, anasema waliwafika Polisi Bunju saa 3:36
asubuhi na kumkuta Dk Ulimboka akiwa amekalishwa kwenye benchi huku damu
ikiwa imeganda kwenye majeraha mwilini.
Olengurumwa anasema
waliwahoji polisi waliokuwa kituoni hapo kwa nini wakae na mtu aliyeumia
kiasi hicho muda mrefu bila ya kuita gari la wagonjwa kumchukua ili
kuwahi kupatiwa matibabu.
Olengurumwa anasema polisi walisema kwamba, walikuwa wanawasubiri ndugu zake wafike.
Baada ya muda mfupi, akiwa ameingizwa kwenye gari kupelekwa hospitali,
Dk Ulimboka aliomba maji ya kunywa akisema ana kiu sana, lakini
alipopewa, alikunywa kidogo akashindwa.
Anasema wakiwa njiani,
alikuwa akilalamika kuwa anasikika maumivu makali huku akisisitiza kuwa
tukio la kutekwa na kupigwa lilikuwa la kumuua.
"Jamani hawa
watu walitaka kuniua walikuwa wamepanga kuniua," alisikika mara kwa mara
akisema Dk Ulimboka wakati anapelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
kupatiwa matibabu.
Maelezo ya Dk Ulimboka
Baada ya
Dk Ulimboka kuokotwa aliweza kuzungumza na kurekodiwa muda mfupi baada
ya kutolewa msituni na mazungumzo yake yalikuwa hivi;
“Nilikamatwa na watu hao usiku wa Jumanne nikiwa maeneo ya Leaders Club,
Kinondoni na daktari mwenzangu baada ya kupigiwa simu na mtu mmoja
ambaye alidai kuwa anafanya kazi Ikulu.
“Kuna jamaa mmoja
anafanya kazi Ikulu, kama siku tatu mfululizo alikuwa akitaka kukutana
na mimi ila nilishindwa kukutana naye kwa kuwa nilikuwa na kazi nyingi
na wakati mwingine mpaka usiku,” alisema Dk Ulimboka.
Huku akizungumza kwa taabu kutokana na mdomo wake kuvimba, alisema siku hiyo mtu huyo alimpigia tena simu na kumtaka wakutane.
“ Jana (Jumanne) alinipigia simu na nikamwambia daktari mwenzangu
twende tukaonane naye, wakati huo alitueleza kuwa alikuwa maeneo ya
Kinondoni Stereo,” alisema Ulimboka na kuongeza:
“Tulipofika
maeneo hayo tukampigia simu na akatueleza kuwa alikwisha ondoka, baadaye
tukamweleza sehemu tulipo mimi pamoja na mwenzangu.”
Alisema kuwa, wakati anakutana na mtu yule maeneo ya Leaders Club, hakuwa na amani.
“Kwa kweli siku ile nilivyoonana na mtu yule sikuwa na amani kabisa ya kukaa eneo lile,” alisema Dk Ulimboka.
Alisema kuwa wakati wakiendelea na maongezi ya kawaida, bado aliendelea kuwa na mashaka na mtu yule.
“Katikati ya maongezi nikaona ameanza kuzungumza na simu, kila tukitaka
kuagana alikuwa akizungumza na simu, sijui nini kilikuwa kinachelewesha
sisi kuagana,” alisema Dk Ulimboka na kuongeza:
“ Ghafla walitokea watu kama watano na kusema kuwa hawana tatizo na mtu yeyote katika eneo hilo isipokuwa mimi.
Wakati sijakaa sawa, waliniburuza hadi barabara ya lami kwa kuwa eneo hilo lilikuwa karibu na barabara.”
Aliongeza, “Nilipowauliza wananipeleka wapi, wakaniambia kuwa mimi
nasumbua sana na nitajua hukohuko, waliniingiza katika gari jeusi,
lakini halikuwa na namba. Niliwauliza kosa gani nimefanya? Hawakunijibu
kitu na kusema, we twende utajua hukohuko.’’
Alisema alipokuwa
ndani ya gari hilo watu hao walimpiga na kwamba walipofika maeneo ya
Victoria, walichukua sweta nyeusi na kumfunga usoni, jambo lililomfanya
ashindwe kuona kinachoendelea ikiwa ni pamoja na alikokuwa akipelekwa.
“Walinipiga mateke ya mbavuni, wakati mwingine walitumia vitako vya
bunduki, kila nilipokuwa najaribu kuangalia ninapokwenda nilishindwa,”
alisimulia Dk Ulimboka.
Alisema kuwa watu hao walimpeleka
katika nyumba moja ambayo hakujua iko sehemu gani ambapo walimshusha na
kuanza kumshambulia kwa mateke mfululizo kila sehemu ya mwili. Wakati
huo, wote walimshinikiza awaambie nani yupo nyuma ya mgomo wa madaktari.
“Tangu saa sita usiku mpaka saa 9:00 alfajiri walikuwa wananipiga tu,
kuna wakati nilijaribu kukimbia wakapiga risasi juu nikasimama na
sikuweza kukimbia tena,” alisema Dk Ulimboka na kuongeza:
“Nilisimama, wakaendelea kunipiga, niliwasikia wakisema ama wanichome
sindano ya sumu nife au kunikanyaga na gari. Baadaye wakaanza kuning’oa
meno na kucha kwa kolea huku wakinilazimisha kusema nani yupo nyuma ya
mgomo wa madaktari."
Alisema kuwa, watu hao walikuwa na bunduki kubwa ambayo hakuweza kuitambua ni aina gani.
“Waliniambia kuwa ninajua ninachokifanya hivyo wanaweza kunichoma
sindano ya sumu nife au wanikanyage na gari nife,” alisimulia.
Dk Ulimboka alisema kuwa awali hakuwa na shaka na watu hao kwa kuwa
alidhani ni polisi, lakini baadaye alishindwa kuwaelewa kwani watu hao
walimchanganya.
“Sikuweza kuwatambua ila naweza kusema ni
askari, walipokuwa wananipeleka niliwauliza mnanipeleka wapi na wakati
huo nilikuwa sioni mbele ila ilikuwa kama maeneo ya Mwenge hivi,”
alisema Dk Ulimboka.
Alisema kuwa baadaye alipoteza fahamu na hakuweza kuona chochote zaidi ya kusikia sauti za watu hao kwa mbali.
“Nilikuwa sioni na nilipoteza fahamu nikawa nasikia tu wakinibeba, gari
lilitembea muda mrefu, sikujua ni wapi tunakwenda, kumbe ndio huko
Mabwepande,” alisema.
Alisema kuwa walifika maeneo ya barabara ya vumbi na baadaye wakamshusha na kumbeba hadi msituni.
“Waliniburuza na kuniacha huko na muda wa saa kumi alfajiri ndipo
nikazinduka na kuanza kujiburuza kuelekea barabarani ambako nilisaidiwa
na mtu mmoja ambaye simtambui,” alisema Dk Ulimboka.
· · Share
NAMNA DOKTA ULIMBOKA ALIVYOKAMATWA NA KUTESWA KINYAMA.
Reviewed by Majuto Omary na Frank Balile
on
9:51 AM
Rating: 5
No comments