Yanga mwendo mdundo, yaichapa Express 2-1, Tegete shujaa
KAMA si juhudi zako Manji, Kama si
juhudi zako Manji, leo hii Yanga ingekuwa wapiiiii. Hicho ni kibwagizo cha
wimbo kilichokuwa kikiimbwa na watani wao wa jadi, mashabiki wa Simba, wakati
wa mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya Yanga na Express ya Uganda.
Mabingwa wa kombe la klabu bingwa
Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), Yanga jana waliibuka na ushindi wa
mabao 2-1 dhidi ya Express, katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliopigwa
Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Wakiwa na furaha, huku wakishuhudia
silaha zao mpya zilizosajiliwa kwa ajili ya Ligi Kuu Bara msimu ujao, Yanga
walianza mchezo kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la kwanza dakika ya tatu
likifungwa na Jerryson Tegete, baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Salum Telela.
Yanga wafanikiwa kupata bao la
pili dakika ya 19, lililofungwa na Tegete kwa kichwa baada ya kazi
nzuri iliyofanywa na Said Bahanuzi.
Bahanuzi aliyetokea Mtibwa Sugar,
aliwapangua mabeki wa Express na kupiga mpira uliosindikizwa wavuni na Tegete
ambaye msimu uliopita alikuwa hachezeshwa mara kwa mara na kocha aliyeondoka
Mserbia Kostadin Papic.
Katika mchezo huo, Express
ilishindwa kuonesha makali yake kipindi cha kwanza, lakini walionekana kuwasoma
zaidi wapinzani wao, ambapo dakika ya 39, walibadilika na kuanza kuonana vizuri
huku wakimjaribu kipa wa Yanga, Ally Mustapha ‘Barthez’ aliyetokea timu ya
Simba.
Express wakiingia kipindi cha pili
wakiwa wamebadilika, walifanikiwa kulifikia lango la Yanga na dakika ya 52,
Joseph Kayira alikosa bao baada ya mpira wa adhabu aliopiga ulipanguliwa na
kipa Barthez na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.
Dakika ya 73, Kayira aliisawazishia
bao timu yake ya Express kwa kichwa akitumia vizuri mpira wa adhabu uliopigwa
na Suleiman Jingo aliyeingia kuchukua nafasi ya Mike Masaba.
Express pamoja na kuonesha kiwango
kizuri cha soka, walikosa mabao matatu kipindi cha pili, huku mashabiki wa soka
wanaokaa upande unaopendelewa na Simba, wakiinua kushangilia wakidhani ni bao.
Mpira huo ulichelewa kuanza baada ya
Express kutaka fedha zao, lakini Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilielewana
nao na kukubali kuingia baada ya kupewa sh. milioni sita na waandaaji wa mchezo
huo.
Express walikuwa wakilalamika kwani
mwaka juzi kampuni moja iliwaalika mkoani Mwanza, lakini mpaka wanamaliza ziara
yao, hawakulipwa fedha walizokubaliana nao, ndiyo maana wakaamua wapewa kabla
ya kuanza kucheza mechi hiyo.
Yanga inajiandaa na mechi za Kombe
la Kagame zitakazoanza Julai 14, mwaka huu jijini Dar es Salaam na Ligi Kuu
Bara.
Mchezo huo ulisimama dakika tatu,
baada ya Stephano Mwasyika kuingia huku akiwa amefungiwa na TFF, baada ya
kumpiga mwamuzi Israel Mujuni, lakini waamuzi waliokuwa wakichezesha mechi
hiyo, baada ya kujadiliana, walimruhusu na kuendelea na mchezo.
Yanga: Ally Mustapha ‘Barthez’, Juma Abdu, Oscar Joshua/Stephano
Mwasyika, Kelvin Yondani, Nadir Horoub ‘Cannavaro, Athuman Idd ‘Chuji’, Nizar
Khalfan/Shamte Ally, Salum Telela, Frank Domayo, Said Bahanuzi, Simon
Msuva/Idrisa Rashid.
No comments