TMK Family kumsindikiza Dogo Aslay
KUNDI zima la TMK Wanaume Family la Temeke
jijini Dar es Salaam, litasindikiza utambulisho wa msanii chipukizi wa muziki
wa kizazi kipya nchini Aslahi Isihaka ‘Dogo Aslay’ litakalofanyika kwenye uwanja
wa Jamhuri Dodoma na ukumbi wa Royal Village mjini humo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jijini
Dar es Salaam jana mratibu wa onesho hilo Jackline Masano wa Kampuni ya Ruhazi
Promotion ya jijini Dar es Salaam, alisema kuwa TMK Family watafanya vituo vyao
kwenye onesho hilo litakalofanyika Jumamosi Juni 9,2012 kwenye uwanja wa
Jamhuri mjini Dodoma.
Alisema TMK Family wanaungana na wasanii kutoka
kituo cha Mkubwa na Wanawe cha Temeke Sandali jijini katika kumsindikiza msanii
huyo aliye gumzo hivi sasa kutona na wimbo wake ‘Naenda Kusema’.
“Tunapenda kuwaambia wapenzi wa muziki wa mjini
Dodoma na maeneo jirani kwamba Kampuni ya Ruhazi Promotion imekubaliana na TMK
Family hivyo mchana wa Jumamosi Juni 09, 2012 kuanzia saa 6:00 mpaka saa 12:00
jioni itakuwa kwenye uwanja wa Jamhuri Dodoma na litaanza saa 2:00 usiku hadi
saa 6:30 usiku kwenye ukumbi wa Royal Village ,” alisema Jackline Masano.
Alisema pamoja na kwamba onesho hilo litapambwa
na wasanii wengi lakini kiingilio kitakuwa shilingi 5,000 tu kwa wakubwa na
shilingi 1,000 kwa watoto ili kuwawezesha wapenzi wengi zaidi kukimudu ambapo
watapata burudani ya uhakika.
Aliongeza kwamba hivi sasa, wanaendeelea
kufanya mazungumzo na wasanii wengine watakaopamba maonesho hayo yote na kwamba
pindi mazungumzo yatakapokamilika watawaweka hadharani.
No comments