Header Ads

ad

Breaking News

TASWA WAMLILIA PATRICK MUTESA MAFISANGO



Wachezaji wa timu ya taifa wakiwa wamebeba jeneza la lililokuwa na mwili wa Mafisango

CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha kiungo wa timu ya Simba ya Dar es Salaam na mchezaji wa timu ya Taifa ya Rwanda (Amavubi), Patrick Mutesa Mafisango kilichotokea  alfajiri ya Alhamisi kwa ajali ya gari jijini Dar es Salaam.
Katibu wa TASWA, Amir Mhando ameiambia BIN ZUBEIRY mchana huu kwamba, wanatoa pole kwa Mwenyekiti wa Simba, Ismail Rage, wachezaji wa timu hiyo, mashabiki na Watanzania kwa ujumla kutokana na msiba huo mkubwa kwa familia ya mpira wa miguu.
"Tunaamini waandishi wa habari za michezo wameguswa kwa kiasi kikubwa na msiba huo, kwani wakati wa uhai wake marehemu alikuwa na ushirikiano mkubwa na wanahabari na hakuwa mtu mwenye maringo, kiasi cha kushindwa kutoa ushirikiano kwa wenzake,"alisema.
Alisema kifo chake ni pigo si kwa  Simba na familia yake tu, bali hata kwa timu ya Taifa ya Rwanda na Wanyarwanda wote, ambao pia tunawapa pole kwa msiba huo.
"Tunawapa pole wanamichezo wote na kuwaomba wawe na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu, huku wakiamini waandishi wa habari za michezo tupo nao pamoja katika majonzi hayo na kumuomba Mungu aiweke roho ya marehemu mahali pema peoni. Amina,"alisema Mhando.
Wakati huo huo: Mhando amesema kuwa mtangazaji wa habari za michezo wa Redio Uhuru, Limonga Justine, amefiwa na baba yake mzazi jana Alhamisi asubuhi kwenye hospitali ya Temeke, Dar es Salaam. alisema msiba upo Mbagala kwa Mangaya, Dar es Salaam na maziko yanatarajiwa kufanyika kesho Jumamosi. Naomba tuungane naye mwenzetu katika kipindi hiki kigumu kwake na tumfariji kwa kadri tuwezavyo kwa kuondokewa na mzazi wake.

No comments