Header Ads

ad

Breaking News

Yanga sasa yanne, yaipiga Coastal Union 5-0

Mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Yanga, leo wamepanda mpaka nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, baada ya kuilaza Coastal Union ya Tanga mabao 5-0, katika mechi iliyopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kwa ushindi huo, Yanga imepiga hatua kubwa kwa kupanda mpaka nafasi ya nne, kwa kufikisha pointi 12, sawa na timu za JKT Ruvu na Mtibwa Sugar, lakini  zinatofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.

Yanga ina tofauti ya mabao matano, wakati JKT ina mabao manne zikiwa sawa, na nafasi ya tatu inashikiliwa na JKT Oljoro ikiwa na pointi 13, huku Azam na Simba, zikikaa kileleni.

Mvua ya mabao ilianza dakika ya nne, baada ya Keneth Asamoah kufunga bao kwa kichwa, akiunganisha krosi ya nzuri Idrisa Rashid, ambaye katika mchezo huo alionekana kutakata zaidi.

Yanga iliendelea kuliandama lango la Coastal Union, na dakika ya 22, Shamte Ally alifunga bao la pili akimalizia krosi iliyopigwa na Asamoah.

Dakika ya 30, Davies Mwape, alifunga bao la tatu akiukwamisha wavuni mpira uliotemwa na kipa Omari Hamis kutokana na shuti lililopigwa na Idrisa.

Dakika ya 41, Nurdin Bakari aliifungia Yanga bao la nne, baada kuonana vizuri na Haruna Niyonzima na Asamoah, kabla ya kurudishwa kwa Nurdin na kufunga.

 Asamoah alifunga bao la tano akiunganisha mpira wa krosi iliotoka kwa Idrisa, ambaye alikuwa akiisumbua sana ngome ya Coastal Union, akiwatoka atakavyo.

Baada ya kufungwa kwa mabao hayo, Yanga ilionekana kuridhika, ambapo katika dakika za 63 na 65 ilifanya mabadiliko kwa kuwatoa Mwape na Asamoah na kuwaingiza Rashid Gumbo na Hamis Kiiza, mabadiliko ambayo yaliounguza kasi ya Yanga.

Coastal ilionekana kama imeamka usingizi, ambapo ilianza kuliandama lango la Yanga na kama washambuliaji wao walioongozwa na Benard Mwalala mchezaji wa zamani wa Yanga wangekuwa makini,  wangepata bao.

Dakika ya 75, Fransis Busungu wa Coastal nusura afunge bao, baada ya shuti lake akiwa ndani ya eneo la hatari, kutua mikononi mwa kipa Yaw Berko, akimalizia pasi ya Mwalala.

Yanga:Berko, Shadrack Nsajigwa, Oscar Joshua, Bakari Mbegu, Nadir Haroub 'Canavaro', Nurdin, Shamte/Julius Mrope, Niyonzima, Mwape/Gumbo, Asamoah/Kiiza na Idrisa.

Coastal:Omar Hamis/Godson Mmasa, Nyumbi/Swed,Soud Juma, Mbwana Hamis, Jamal Machelanga, Mwinyi Abdulrahman, Busungu, Mohamed Ibrahim, Daniel Lianga, Mwalala na Rashid Mandawa.

No comments