Stars kambini Septemba 30
TIMU ya taifa 'Taifa Stars', itaingia kambini Septemba 30, mwaka huu kujiandaa na mechi dhidi ya Morocco ya Kundi D, kuwania kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika, mwakani (CAN 2012).
Taifa Stars ipo nafasi ya tatu kwa pointi tano ikitanguliwa na Morocco na Jamhuri ya Afrika ya Kati, zinazoongoza kwa pointi nane kila moja.
Timu hizo zinaongoza isipokuwa zinatofautiana mabao kufunga, huku Algeria ikiburuza mkia, ikiwa sawa na Stars isipokuwa imezidiwa kwa mabao.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura amesema timu hiyo itaingia kambini baada ya Kocha Mkuu, Jan Poulsen kuwasilisha programu yake na kupendekeza siku ya kuanza kambi.
Amesema nchi nyingi zinajiandaa na mechi za mwisho za fainali hizo, hivyo hadhani kama zitapatikana kiurahisi, lakini watajipanga kuhakikisha timu inaandaliwa vizuri kwenda kuumana na Morocco.
Mechi za kundi hilo zitachezwa saa 1.30 jioni siku moja ambayo ni Oktoba 9, mwaka huu ili kuepusha kupanga matokeo ambapo Taifa Stars, itakuwa jijini Rabat na Algeria itaumana na Jamhuri ya Afrika ya Kati Jijini Algiers.
Waamuzi wa mechi hiyo kati ya Stars na Morocco watakuwa ni Gassama Bakary, Jawo Dickory, Touray Sulayman na Camara Bakary, wote kutoka Gambia. Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Zoumaro Gnofame kutoka Togo.
No comments