Header Ads

ad

Breaking News

Elimu ya Shinikizo la juu la damu yatolewa katika maonesho na madini Geita

Afisa Utafiti na Mafunzo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Zabela Mkojera, akimpima urefu na uzito mwananchi aliyetembelea banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika Maoneshoi ya Nane ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika viwanja vya Maonesho vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mjini Geita.

Na Jeremia Ombelo, Geita

TATIZO la ugonjwa wa shinikizo la damu waelezwa kuongezeka kwa vijana huku idadi kubwa ya vijana hao kuishi na tatizo hilo bila ya kuonyesha dalili zozote.

Hayo yamesema na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Henry Mayala, wakati wa maonesho ya nane ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika Viwanja vya Maonesho vya Dkt. Samia Suluhu Hassan vilivyopo mjini Geita.

Dkt. Mayala amesema kulingana na takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kuwa zaidi ya watu bilioni 1.3 duniani wanaishi na ugonjwa wa shinikizo la damu huku asilimia 46 ya watu hao wana umri wa kuanzia miaka 25.

“Wananchi wanatakiwa kupima afya zao mara kwa mara ili kujua kama wana tatizo la shinikizo la damu, na kwa wale waliopimwa na kukutwa na ungonjwa huu wanatakiwa kupimwa mara tatu kwa siku tatu tofauti kuthibitisha kuwa wana ugonjwa huo,” amesema Dkt. Mayala.

Afisa Utafiti wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Makrina Komba akimpima shinikizo la damu mwananchi aliyetembelea banda la hiyo lililopo katika Maonesho ya Nane ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika viwanja vya Maonesho vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mjini Geita.

Dkt. Mayala ameongezea kuwa watu wengine hupata dalili kama vile uchovu usio wa kawaida, jasho jingi, na maumivu ya kichwa sehemu ya nyuma ya kichogo lakini bado utawakuwa hawafuatilii afya zao.

“Asilimia kubwa ya watu wenye shinikizo la damu mara nyingi hawana dalili, tafiti zinaonyesha kati ya wagonjwa kumi wagonjwa sita wana tatizo la shinikizo la damu na wagonjwa hawa wapo ambao wanajijua na wengine hawajijui,” amesema Dkt. Mayala.

Dkt. Mayala amesema kuna haja ya kuwekeza kwenye elimu ya afya kwa jamii ili kuondoa mitazamo potofu na kukuza utamaduni wa kupima afya mara kwa mara hasa kwa wale ambao hawana dalili zozote lakini wako kwenye hatari.

Baadhi ya wananchi waliotembelea banda la taasisi hiyo walishukuru kwa kupata elimu na kuona umuhimu wa kufanya uchunguzi wa afya zao mara kwa mara.

Baadhi ya wananchi wakisubiri kupata huduma za vipimo na matibabu ya moyo walipotembelea banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kupata huduma hizo katika Maonesho ya Nane ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika viwanja vya Maonesho vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mjini Geita.

“Nimepata elimu ya kutosha kuhusu shinikizo la juu la damu, ninawashukuru madaktari kwa kutupa elimu hii muhimu,” amesema Nelson Simon Mkazi wa Geita.

“Madaktari wamenifundisha kuhusu ulaji bora kuepuka matumizi ya chumvi nyingi na umuhimu wa mazoezi ili kuepukana na magonjwa ya moyo,” amesema Laurencia Bujashi mkazi wa Geita.

No comments