Wawekezaji waitikia wito wa Rais Samia uongezaji thamani madini nchini
*Waziri Mavunde azindua kiwanda cha kuongeza thamani madini chumvi
*Ni cha uzalishaji chumvi lishe kwa ajili ya mifugo
*Lengo ni kupunguza uagizaji wa chumvi lishe nje ya nchi
*Tanzania kuongeza uzalishaji wa chumvi ghafi kwa matumizi ya viwandani
Mwandishi Wetu, Uvinza
WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde, ameipongeza Kampuni ya Nyanza Salt kwa kuitikia wito wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, wa uongezaji thamani madini nchini kwa kuanza rasmi uzalishaji wa chumvi lishe itokanayo na madini ya chumvi mahsusi kwa ajili ya kuongeza virutubisho vya mifugo.
Mavunde ameyasema hayo leo Ijumaa Agosti 15,2025 wilayani Uvinza mkoani Kigoma, wakati akizindua shughuli za Kiwanda cha kuzalisha chumvi lishe kwa ajili ya mifugo kinachomilikiwa na Kampuni ya Nyanza Salt.
“Ni wito wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na matakwa ya sheria juu ya uongezaji thamani madini yetu nchini.
"Nawapongeza Kampuni ya Nyanza kwa hatua hii kubwa ya kuitoa chumvi yetu katika matumizi ya kawaida na kuiongezea thamani kuzalisha chumvi lishe, ambayo ni muhimu kwa virutubisho vya mifugo."
"Wafugaji wengi huagiza chumvi lishe kutoka nje ya nchi kwa kuwa, hatukuwa na uzalishaji hapa nchini, hatua hii ya leo ya uzalishaji wa 𝘾𝙖𝙩𝙩𝙡𝙚 𝙇𝙞𝙘𝙠 nchini, itapunguza uagizwaji wa bidhaa hii kutoka nje ya nchi kwa kiwango kikubwa, hivyo natoa rai kwa wafugaji kuiunga mkono bidhaa hii inayozalishwa ndani ya ya nchi," amesema Waziri Mavunde.
Tasnia ya chumvi inaendelea kukua kwa kasi siku hadi siku na lengo la serikali ni kuhakikisha wanaboresha mazingira ya uwekezaji kwenye eneo hilo, ili kuongeza tija na uzalishaji na kuondokana kabisa na uagizaji wa chumvi ghafi nje ya nchi kama malighafi ya viwanda.Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Nyanza Salt Mines, Mukesh Mamlani, amesema uzalishaji wa bidhaa ya chumvi lishe itokanayo na madini chumvi ni mkombozi kwa wafugaji wa Tanzania na kwamba, kampuni hiyo itahakikisha inakidhi viwango na ubora wa bidhaa ili wafugaji wa Tanzania wanufaike.
Mukeshi ameeleza kwamba, mpango wa kampuni yao ni uzalishaji wa tani 120,000 za chumvi ifikapo mwaka 2027 ili kuhakikisha inakuwa ya kutosha na kupatikana nchini kote.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Dina Mathamani, amesema uwepo wa Kampuni ya Nyanza wilayani Uvinza umekuwa ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi na mapato kwa serikali na wananchi, ambapo kupitia ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja jumla ya wananchi 1,000 wamekuwa wakipata ajira kiwandani hapo wakati wa msimu wa uchakataji chumvi.
No comments