Jumaa awaahidi Wajumbe uwanja wa michezo
Mgombea ubunge Jimbo la Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani, Humoud Jumaa
Na Omary Mngindo, Mlandizi
MGOMBEA ubunge Jimbo la Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani, Humoud Jumaa, amewaahidi wajumbe wa kura za maoni kuwa, jina lake likirudi, pamoja na shughuli za maendeleo pia ataangalia upatikanaji wa viwanja vya michezo.Jumaa alijibu swali la mjumbe aliyehoji changamoto hiyo, wakati Kamati ya Siasa ikiongozwa na Mwenyekiti Mkali Kanusu, Katibu Ezekiell Mollel na viongozi wengine walipowatembeza katika Kata mbalimbali watia nia ya nafasi hiyo.
Msafara ukiwa Kata Mtambani baada ya wagombea hao wakijinadi mbele ya Wajumbe kwenye Jengo la Chama Cha Mapinduzi lililopo Kitongoji cha Said Domo, Mjumbe huyo alimuuliza kama akipita kilio cha uwanja atakichukukuliaje.
Akijibu swali hilo Jumaa alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo, huku akiongeza kuwa ukiachia uwanja wa michezo pia hata viwanja kwa ajili ya sherehe mbalimbali hakuna, na kwamba mbali ya shughuli za kimaendeleo pia atalivalia njuga suala hilo.
"Vijana wetu hawana eneo la uwanja wa michezo, na sio hilo pekee pia hata Viwanja kwa ajili ya sherehe mbalimbali zikiwemo za Sikukuu, hali inayowanyima watoto kwenda kusherehekea sherehe hizo," alisema Jumaa.
Mchakato huo wa nafasi hiyo ukiwaniwa na mgombea anayetetea nafasi hiyo Michael Mwakamo na Eli Achahofu, chini ya Kamati hiyo walitembezwa katika Kata zote 11 zinazounda Jimbo hilo.
Katika mchakato huo wa kura za maoni uliofanyika Agosti 4 mtia nia huyo aliibuka kinara kwa kujikisanyia kura 3,247 dhidi ya Mwakamo kura 1,802 huku Achahofu akikusanya kura 178.
No comments