TADB yang'arisha maonuesho ya nanenane milioni 400
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
BENKI ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), imemshukuru Rais Samia Sulunu Hassan kwa kuipatia fedha nyingi ambazo zimeiwezesha kuwakopesha wakulima wengi na hatimaye kutangazwa kuwa, mionghoni mwa benki kubwa nchini
Benki hiyo ndiyo imekuwa mdhamini mkuu wa maonesho ya wakulima ya Nane Nane yanayoanza leo kwenye viwanja vya Nane Nane mkoani Dodoma, ambapo Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango, anatarajiwa kuyatembelea.
Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Frank Nyabundege, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maonesho hayo na udhamini wa Shilingi milioni 400 wa benki hiyo kwenye maonesho hayo.
Amesema TADB imeamua kudhamini maonesho hayo kama sehemu ya shamrashamra za kusherehekea miaka 10 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2015 na mafanikio makubwa waliyopata.
Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema TADB imefanya mambo makubwa kwenye sekta ya kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi na sekta mbalimbali za serikali.
Amesema benki hiyo imeamua kudhamini maonesho hayo kwa kuwa, yenyewe ndiyo kinara wa utoaji wa mikopo kwenye sekta ya kilimo.“Sisi ndiyo kinara wa mikopo ya sekta ya kilimo kwasababu tunawakopesha wakulima wengi sana, na mwaka huu tumehitimu kuwa miongoni mwa benki kubwa nchini,”amesema
“Benki zimewekwa kwenye makundi matatu, benki ndogo, benki za kati na kubwa, sisi tulianza na mtaji mdogo, lakini mwaka huu tumeingizwa kuwa benki kubwa nchini baada ya mizania yetu kuzidi trilioni moja,” amesema
“Mtu anaweza kuhoji mmefikaje mbali kiasi hicho ndani ya muda mfupi wakati kuna benki zimekaa miaka zaidi ya 20, lakini bado hazijafikia kuwa benki kubwa, jibu ni kwamba tumefika hapa kutokana na utashi wa kisiasa wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa akituongezea mtaji mwaka hadi mwaka,” amesema
Amesema Rais Dkt. Samia alipoingia madarakani aliweka kipaumbele kuimarisha na kuboresha sekta ya kilimo na alifanya hivyo kwa kufahamu kuwa, sekta hiyo ndiyo inaajiri asilimia sabini ya wakulima.
“Rais Samia ametambua kuwa, ukigusa sekta ya kilimo umegusa maisha ya watanzania wengi na ndiyo sababu kwa muda wote amekuwa akiwekeza kwenye sekta ya kilimo ili kuiinua sekta hii na kuinua kipato cha watanzania,” amesema.
Nyabundege amesema wakati akiingia madarakani, Dkt.Samia alikuta bajeti ya kilimo ni Sh.bilioni 264, lakini kwenye utawala wake bajeti hiyo imepanda hadi kufikia trilioni 1.2.“Alipoingia madarakani TADB ilikuwa na mtaji wa Sh.bilioni 60, lakini ametuongezea mtaji wa Sh. bilioni 442 na riba asilimia 20 mpaka 30, akaweka Sh.trilioni moja Benki Kuu (BoT), kama dhamana ya kuchachua uchumi ili benki za biashara zikopeshe sekta ya kilimo chini ya asilimia 10,” amesema.
No comments