Rais Samia azitaka wizara kutoa huduma za kibandari Kwala
Na Mwandishi Wetu, Pwani
RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan amezitaka Wizara za Uchukuzi na Viwanda na Biashara kuanza kutoa huduma zote za kibandari katika Bandari Kavu ya Kwala ili kurahisisha shughuli za usafirishaji kuanzia Agosti 4, 2025.
Maagizo hayo ameyatoa leo wakati wa uzinduzi wa Bandari Kavu ya Kwala iliyopo mkoani Pwani, huku akisema ni hatua ya kihistoria itakayopunguza gharama za usafirishaji, kuondoa msongamano wa malori jijini Dar es Salaam, pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi, uwekezaji wa viwanda na ajira kwa wazawa.
Dkt. Samia amesema uzinduzi wa kituo hicho utarahisisha shughuli za uchukuzi na kupanua wigo wa biashara kwa watanzania na nchi jirani, ambapo kituo hicho kitaifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, ikiwa ni maandalizi ya ushiriki kamili wa nchi katika Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).
Amesema Bandari Kavu ya Kwala itarahisisha usafirishaji wa mizigo ya nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Zambia, Burundi, Rwanda na Malawi na kuongeza mvuto wa Bandari ya Dar es Salaam katika ushindani wa kikanda," amesema Dkt. Samia.
Rais Dkt. Samia amezindua rasmi safari za mizigo za treni ya umeme ya SGR, na kusema kwamba hatua hiyo muhimu itabadili rnfumo wa uchukuzi nchini, ambapo ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kupunguza gharama za usafirishaji, uchakavu wa barabara na kulinda mazingira."Serikali imewekeza Sh.bilioni 330.2 kwa ajili ya ununuzi wa mabehewa 1,430 ya mizigo, lengo likiwa ni kuongeza ufanisi na kupunguza gharama kwa wafanyabiashara. Natoa wito kwa sekta binafsi kutumia fursa ya uwepo wa reli hii kuwekeza katika usafirishaji wa mizigo na abiria, ikiwemo kununua vichwa na mabehewa yao wenyewe."
Rais Dkt. Samia ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Kongani ya Viwanda ya Kwala inayotarajia kuwa na viwanda 200 itakapokamilika, viwanda saba tayari vimeanza kazi na vitano vipo katika hatua ya ujenzi.
Akizungumzia fursa za ajira, Dkt.Samia amewataka wananchi wa Mkoa wa Pwani na watanzania kuchangamkia fursa hizo, ikiwemo kuanzisha biashara ndogondogo na huduma zinazozalishwa na mradi huo, akiweka wazi kuwa ajira 50,000 za moja kwa moja na 150,000 zisizo za moja kwa moja zitazalishwa kutokana na viwanda 200 vitakavyojengwa katika Kongani hiyo ya Viwanda.
No comments