Header Ads

ad

Breaking News

Msama awataka watanzania waheshimu mamlaka, awaonya wanaotukana mitandaoni

Mkurugenzi wa Msama Promotion na mwandaaji wa Tamasha la Pasaka, Alex Msama (kulia), akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichana), leo Jumapili Juni 8,2025 jijini Dar es Salaam

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MKURUGENZI wa Msama Promotion na mwandaaji wa Tamasha la Pasaka, Alex Msama, amewataka watu wanaoandika matusi na kutukana mitandaoni  kwa kuwachafua wengine waache mara moja. 

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Msama alisema kuwa nchi yetu inakabiliwa na changamoto nyingi kuelekea uchaguzi mkuu, na ni muhimu kuheshimu mamlaka zilizopo, huku akisisitiza kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameteuliwa na Mungu kwa ajili ya kuwatumikia watanzania.

Msama alisema kwamba, Dkt.Samia anaongozwa na Mungu, na mambo yote anayofanya anaekelezwa na Mungu huku akinukuu kifungu cha Biblia Warumi 13:1 kisemacho, 'Kila mtu na aitii mamlaka kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo umeamriwa na Mungu.'

'Hivyo amwasiye mwenye mamlaka hushindana na agizo la Mungu; nao washindanao watajipatia hukumu.'

Msama alisema Rais Samia anakaribia kumaliza kipindi cha miaka minne ya uongozi wake, hivyo anatarajiwa kuingia awamu ya pili baada ya uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu, huku akiwataka wananchi, hasa wanaojihusisha na dini, kumheshimu Rais na mamlaka zake.

Alisema siasa hazipaswi kuchanganyikana na mambo ya ibada, na kuwataka baashi ya viongozi wa dini, wanaoingiza siasa ndani ya nyumba za ibada, waache kwani wanaweza kuhatarisha amani.

“Siasa si sehemu ya ibada, nyumba za ibada ni mahali pa kumuabudu Mungu, iwe ni kanisani au msikitini,  na ndiyo maana tunawaomba viongozi wetu wa dini walizingatie hilo," alisema.

Aliongeza kuwa, kama kiongozi wa dini anataka kuzungumzia siasa, ni muhimu kwa watumishi wa Mungu kuelewa majukumu yao na kujitenga na mambo ya siasa.

Msama alisema kuwa, watumishi wanaochanganya siasa na Mungu makanisani, wanamkosea sana Mungu, kwani wanajua Mungu amewakataza kuchanganya siasa na dini, wanatakiwa kuhubiri injili ya Mungu ili watu waache maovu na kumgeukia Mungu.

"Watu wakiacha maovu na kumgeukia Mungu, serikali itatawala vizuri na watu wataendelea kufanya shughuli zao, tunasafiri kwenda sehemu yoyote, tunalala hotelini kwa usalama, hiyo ndiyo kazi Mama Samia aliyopewa na Mungu aifanye,"alisema.




No comments