Alhaj Nassoro awaasa wana Chalinze kuelekea Idi
Na Omary Mngindo, Chalinze
KIONGOZI wa Maimamu Jimbo la Chalinze, Halmashauri ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, Alhaj Hamisi Nassoro, amewataka wana Chalinze kushiriki Sikukuu ya Idi Al-haji kwa amani na utulivu.
Alhaj Nassoro alisema kuwa katika kuelekea kwenye sikukuu hiyo kubwa ni vema wana Chalinze, Bagamoyo na waTanzania kwa ujumla wakaendelea kudumisha amani, umoja, upendo na mshikamano.
"Watanzania tuna utamaduni wetu wa kuheshimiana katika vipindi vyote, hivyo nitumie nafasi hii tukielekea kwenye sikukuu ya Idi Mfungo Tatu tukaendeleza utamaduni wetu wa kupendana na kudumisha amani yetu," alisema Alhaj Nassoro.
Aidha, amewataka waumini na wa Tanzania kuendelea kuiombea nchi pamoja na viongozi wake, hasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Ameongeza kuwa "Serikali yetu inaendelea kutusogezea huduma za kijamii kwa karibu zaidi, tunashuhudia ujenzi wa zahanati, vituo vya afya, hospitali, shule, barabara, umeme na maji," alisema Alhaj huyo.
Amefafanua kuwa, nchi yetu iko kwenye neema kubwa ya utulivu, hivyo wasikubali amani hiyo kuchezewa na kwamba ni wajibu wa kila mtanzania kuilinda amani iliyopo.
"Niwaombe tuendelee kudumisha umoja upendo na mshikamano wetu kwa watu wote, ili tuendelee kuishi katika mazingira ya kumpendeza Mwenyeezimungu," alimalizia Alhaj huyo.
No comments