TRA SC WATWAA KOMBE LA DSSL MARA YA PILI MFULULIZO , SASA MABINGWA WA KIHISTORIA
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
TIMU ya soka ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ya TRA SC imefanikiwa kutetea ubingwa wake wa kombe la wafanyakazi Dar es Salaam (Dar Es Salaam Staff Sports League' (DSSL) kwenye mchezo wa fainali dhidi ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) ushindi wa bao 1-0.Mchezo huo wa fainali ulichezwa katika Uwanja wa TRA Kurasini Aprili 5, 2025 ulishuhudiwa na shamrashamra na shangwe mbalimbali kwa mashabiki wa timu zote mbili, ulikuwa wa kuvutia licha ya mvua iliyokuwa iliyonyesha dakika 45 za kwanza za mchezo huo,
Hata hivyo TRA SC walifanikiwa kupata bao kipindi cha pili, lilidumu mpaka mwisho wa mchezo huo na kuwafanya kuwa mabingwa wapya wa kihistoria kwa kutwaa ubingwa mfululizo, wakifanya hivyo mwaka jana na mwaka huu 2025.
TRA wameweka rekodi ya kipekee kwa upande wa timu ya netiboli walitwaa ubingwa dhidi ya Bohari Kuu ya Dawa (MSD), na kutwaa ubingwa kwa mara ya pili mfululizo.
Awali, akikabidhi zawadi za ushindi, mdau wa michezo na mwanamichezo nchini Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya, Dkt. Jonas Tiboroha kwa niaba ya Mkurugenzi wa Michezo BMT, alipongeza vipaji vya wachezaji wa timu zote huku akiomba maafisa uajili kuendelea kuwekeza zaidi michezoni kwani inasaidia wafanyakazi kuwa vyema kiafya na ufanisi kazini.
"Niwapongeze viongozi wa timu zote bahati nzuri mpo hapa. Michezo inasaidia ufanisi, inapunguza hata bajeti ya matibabu, tuendelee kuwekeza kwenye michezo na tuangalie namna ya kuweka sawa miundombinu ya michezo,"alisema Dkt.Toboroha na kuipongeza TRA kwa ujenzi wa uwanja huo wa Kurasini, hali inayowapa ufanisi mkubwa kwa kushinda makombe katika michuano mbalimbali ikiwemo SHIMUTA na mingine mingi ya Wafanyakazi nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa mashindano hayo, Japhari Saidi Mtoro amezipongeza timu zote kwa hatua waliyofikia, huku akiahidi msimu ujao mambo makubwa.
"Mashindano ya wafanyakazi lazima yalindwe kwa nguvu na wivu mkubwa, hivyo ni muhimu kuwekeza katika mifumo itakayozuia mtu yeyote asiye na sifa kushiriki mashindano hayo.
Akifafanua zaidi, mwenyekiti huyo alisema kuanzia msimu unaokuja wataweka mfumo wa biometric utakaotumika kuwasajili na kuwatambua wachezaji kwa sura zao na alama za vidole.
Mashindano hayo yalishirikisha timu 14, zilizocheza mfumo wa ligi, kila wiki ilikujenga afya ya watumishi wachezaji maofisini, lakini pia kujiandaa na michezo mbalimbali pahala pa kazi.
No comments