Shilingi bilioni 800 kupanua, kujenga kiwanda cha saruji
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SERIKALI kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina na kampuni ya AMSONS ya Uswisi, wameingia makubaliano ya kuwekeza dola milioni 320, zaidi ya sh.bilioni 800 katika upanuzi wa kiwanda cha Saruji Mbeya na kuanzisha kiwanda kipya cha saruji Tanga.
Hayo yamesemwa Oktoba 15 jijini Dar es Salaam na Msajili wa Hazina, Bw.Nehemiah Mchechu, wakati wa mkutano na waandishi wa habari.
Bw.Mchechu anasema kati ya fedha hizo, dola milioni 190 sawa na sh.bilioni 513 zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda kipya Tanga na dola milioni 130 sawa na sh. bilioni 351 ni kwa ajili ya upanuzi wa kiwanda cha Saruji Mbeya.
“Hivi ninavyozungumza tayari tumeshafanya maamuzi ya kimsingi. Kazi zilizobakia ni za kimenejimenti, ikiwemo kumalizia mpango wa biashara na hatua nyingine za kifedha,” alisema Bw.Mchechu.
Anasema mradi huo wa upanuzi wa kiwanda cha saruji Mbeya na ujenzi wa kiwanda kipya Tanga, unaotarajiwa kukamilika ndani ya miaka miwili hadi mitatu, utachangia kuongezeka kwa uzalishaji wa klinka mara 10.
Kwa kiwanda cha Mbeya, anafafanua, uzalishaji wa klinka, malighafi muhimu kwa utengenezaji wa saruji, unatarajiwa kuongezeka kutoka tani 1,000 kwa siku hadi kufikia tani 5,000.Anaendelea kufafanua kuwa, kwa upande wa kiwanda kipya cha Tanga, kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 5,000 za klinka kwa siku.
“Kuongeza kwa uzalishaji kutatufanya tuendelee kulikamata vizuri soko la nyanda za juu kusini ambalo tumekuwa tukilihudumia kwa zaidi ya asilimia 70 kwa muda mrefu,” anasema Bw.Mchechu.
Anaongeza: “Uwekezaji huu pia utakuwa mwanzo wa kupenye kwenye nchi jirani za Zambia, Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.”
Bw.Mchechu alnasema uwekezaji huo ni matokeo ya uboreshwaji wa mazingira rafiki ya biashara na uwekezaji yanayofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
“Uwekezaji huu ni sehemu ya mabadiliko ambayo Mhe.Rais amekuwa akitamani kuyaona katika mashirika ambayo serikali ina hisa,” anasema.Kwa upande wake Mkurugezi wa Fedha wa AMSONS Bw.Ahmed Mhada alisema kukamilika kwa mradi wa upanuzi na ujenzi wa kiwanda kipya kutachangia kuongezeka kwa uzalishaji wa saruji kutoka tani milioni 1.1 kwa mwaka hadi kufikia tani milioni 4.2.
“Inatarajiwa kuongezeka kwa uzalishaji kuchangia kuongezeka kwa gawio mara 10 ya lile ambalo serikali ilipata mwaka jana,” anasema Bw.Mhada.
Serikali, ambayo inamiliki asilimia 25 ya hisa, kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, mwaka jana ilipata gawio la sh. bilioni 3, ikiwa ni miaka 10 ipite bila kampuni hiyo kutoa gawio.
Kama ongezeko la uzalishaji linatarajiwa kuongeza gawio mara 10, tafsiri yake ni kuwa, serikali inatarajia kuanza kupata sh. milioni 30 kama gawio baada ya mradi kukamilika.
Kwa upande wa ajira, Bw.Mhada, anasema kuwa, kukamilika kwa mradi huo, kutazalisha ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja 12,000.
Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Kiwanda cha Saruji Mbeya, Prof.Siasa Mzenzi, anamshukuru Mhe.Rais kwa kutengeneza mazingira rafiki ya biashara na uwekezaji nchini.“Anachofanya Mhe.Rais, kinavutia wawekezaji kuwekeza nchini. Tuko tayari kusimamia uwekezaji huu ipasavyo kwa maslahi mapana ya taifa letu na watu wake,” anasema Prof.Mzenzi.
Kadri siku zinavyozidi kwenda, idadi ya watu inazidi kuongezeka, na hatimaye mahitaji ya saruji yanazidi kupaa.
Mpaka kufikia Desemba mwaka jana, uzalishaji wa saruji Tanzania ulikuwa tani milioni 11 ikilinganishwa na mahitaji ya tani milioni 7.5.
Kiwanda cha Saruji cha Mbeya kinamilikiwa kwa ubia kati Kampuni ya Amsons kutoka Holcim ya Uswisi asilimia 65, serikali ya Tanzania kupitia kwa Msajili wa Hazina asilimia 25 na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) wenye hisa asilimia 10.
No comments