Header Ads

ad

Breaking News

MWENYEKITI WA BODI NCAA ATEMBELEA ONESHO LA SITE 2024 NA KUPONGEZA JUHUDI ZA KUTANGAZA UTALII


Na Hamis Dambaya, NCAA

MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Jenerali Venance Mabeyo (Mstaafu), ametembelea banda la mamlaka hiyo katika Maonesho ya Kimataifa ya Swahili International Tourism Expo 2024 yanayofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar esalaam.

Ameipongeza menejimenti kwa kuendelea kufanya kazi kwa juhudi na maarifa katika kuendeleza uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii.

Katika banda la NCAA, Mwenyekiti huyo wa bodi alipokea maelezo ya ushiriki wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro katika maonesho hayo kutoka kwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi anayeshughulikia huduma za utalii na Masoko Bi. Mariam Kobelo, alisema kuwa ushiriki wa maonesho hayo unasaidia kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kufanya utalii katika hifadhi hiyo.

Bi. Kobelo amesema kuwa, wageni wengi wanaofika katika banda hilo hupata nafasi ya kuelezwa vivutio mbalimbali vilivyopo katika Hifadhi ya Ngorongoro, ambapo wanaotembelea hifadhi hiyo wanaona wanyama mbalimbali kama vile samba, tembo, chui, faru, nyati, swala, twiga na wengine.

Aliongeza kuwa, pia hupata nafasi ya kujua historia ya binadamu kupitia makumbusho ya Olduvai Gorge, kuona mchanga unaohama, nyayo za zamadam na vinginevyo vingi.

"NCAA tutaendelea kutumia maonesho mbalimbali katika kujitangaza na njia hii imekuwa ikisaidia kuongeza wigo wa watalii wa ndani na wa kimataifa, jambo ambalo limesaidia sana kuongezeka kwa idadi ya wageni wanaotembelea hifadhi hiyo,” ameongeza Kobelo.

Onesho la kimataifa ya SITE huwakutanisha wadau wa sekta ya utalii kutoka ndani na nje ya nchi, pamoja na mambo mengine husaidia kukuza utangazaji wa utalii, huku wadau mbalimbali hukutana kwa pamoja chini ya mwamvuli wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

No comments