Rais Magufuli apokea taarifa ya uhakiki wa vyeti
JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
Simu: 255-22-2114512,
2116898
E-mail: press@ikulu.go.tz
Faksi: 255-22-2113425
|
OFISI YA RAIS,
IKULU,
1 BARABARA YA BARACK OBAMA,
11400 DAR ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 28 Aprili 2017, amepokea
taarifa ya uhakiki wa vyeti kwa Watumishi wa Umma katika ukumbi wa Chimwaga
mkoani Dodoma na kuiagiza Wizara ya fedha kuwaondoa katika orodha ya Watumishi
wa Umma na kusimamisha mishahara ya Watumishi 9,932 waliobainika kutumia vyeti vya
kugushi.
Idadi ya watumishi
hao imebainika baada ya Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mheshimiwa Angela
Kairuki kukabidhi taarifa ya zoezi la uhakiki wa vyeti kwa watumishi wa Umma zaidi
ya laki nne kwa Rais Magufuli, zoezi ambalo liliendeshwa na Serikali kuanzia
mwezi Oktoba mwaka 2016.
Rais Magufuli pia
amewataka Watumishi 9,932 waliobainika kutumia vyeti vya kugushi kujiondoa wenyewe
katika utumishi wa Umma kabla ya tarehe 15 Mei 2017 na baada ya muda huo hatua
za kisheria zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kufikishwa katika vyombo vya
sheria.
'' Kwa hiyo Waziri
Mkuu upo hapa na Waheshimiwa Mawaziri wote mnaohusika, hawa watu 9932 mshahara
wao wa mwezi huu ukatwe na waondoke mara moja kwenye Utumishi wa Umma kuanzia
leo, watakao baki mpaka tukiingia mwezi wa tano tuwapeleke kwa mujibu wa sheria
ili kusudi wakafungwe hiyo miaka saba'' amesema
Rais Magufuli.
Pia Rais Magufuli ameiagiza
Wizara ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora kutangaza nafasi hizo
9,932 upya ili wenye sifa stahiki waweze kuomba
Aidha, Rais
Magufuli ameiagiza Tume inayofanya uhakiki wa vyeti kwa Watumishi wa Umma kwa
kushirikiana na Wizara ya Elimu kuendelea na uchunguzi wa Watumishi wa Umma 1538 waliobainika kutumia
vyeti vyenye utata hadi Mei 15, 2017
''
hawa
wenye vyeti vya utata kwa maana kuwa vyeti vyao
vinatumiwa na watu zaidi ya mmoja, Wizara ya Utumishi muhakikishe kufika
tarehe 15 muwe mmeshajua ni nani mwenye cheti chake, na mshahara wa mwezi huu
wasipewe kwanza mpaka atakayepatikana mwenye cheti halali'' amesema
Rais Magufuli.
Pia ameagiza
uchunguzi ufanyike kwa watumishi 11,596 wenye vyeti vya Utaalumu bila kuwasilisha
vyeti vya kidato na Sita kwa kuwa sio fani zote zinazohitaji kuwa na vyeti vya
kidato cha Sita ili kusomea utaalamu husika na kuagiza kulipwa mishahara yao
kama kawaida.
Katika
hatua nyingine, Rais Magufuli amezindua
maadhimisho ya miaka kumi tangu kuanzishwa kwa Chuo kikuu cha Dodoma.
Rais magufuli
amewaelezea Wanajumuiya ya Chuo Kikuu cha Dodoma mipango mbalimbali inayofanywa
na Serikali katika kuboresha maisha ya
Watanzania na kukuza Uchumi ikiwa ni pamoja na kuimarisha Miundombinu ya Usafiri
kwa kununua ndege mpya Sita na Ujenzi wa Reli ya kisasa.
Mheshimiwa Rais
amesema hatua ya Serikali kuimarisha huduma za jamii inatokana na mafanikio ya
Serikali kudhibiti upotevu wa mapato na hivyo kuwataka wananchi kuunga mkono
jitihada za Serikali ili kukamilisha malengo ya Tanzania ya viwanda.
Naibu
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chamwino, Dodoma
28 Aprili,
2017
No comments