TAIFA STARS, MALAWI UWANJANI DAR
Timu za Taifa za Tanzania (Taifa
Stars) na Malawi (The Flames) zinapambana kesho (Mei 26 mwaka huu) katika mechi
ya kirafiki itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili
jioni.
Makocha wa timu zote mbili, Kim
Poulsen wa Taifa Stars na Kinnah Phiri wa The Flames wamezungumzia umuhimu wa
mechi hiyo katika Mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika leo (Mei 25 mwaka
huu) ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Kim ambaye hiyo itakuwa mechi yake
ya kwanza tangu asaini mkataba wa kuinoa Stars, amesema baada ya mazoezi ya
siku kumi hicho ndicho kipimo chake cha kwanza na cha mwisho kabla ya kucheza
na Ivory Coast kwenye mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia itakayofanyika ugenini
Juni 2 mwaka huu.
“Wachezaji wangu wamekuwa wakipokea
mafunzo vizuri ingawa Nurdin Bakari na Thomas Ulimwengu hatakuwepo kwa vile ni
majeruhi. Bila shaka baada ya mazoezi ni lazima ujipime, hivyo mechi hii ni
muhimu kwangu ukizingatia kuwa kwenye ubora wa viwango vya FIFA, Malawi wako
juu yetu,” amesema Kim.
Naye Phiri ambaye ni mchezaji wa
zamani wa kimataifa wa Malawi amesema awali aliombwa mechi na Misri, lakini
akaamua kucheza na Taifa Stars kwa vile anaamini kitakuwa kipimo kizuri kwake
kabla ya kucheza mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Kenya
itakayofanyika Juni 2 mwaka huu jijini Nairobi.
“Nimekuja na wachezaji 20 ambapo
nusu yao wanacheza mpira wa kulipwa nje ya Malawi, wengi wakiwa Afrika Kusini
lakini wapo pia kutoka Msumbiji na mmoja anacheza Hispania katika timu ya
vijana ya Atletico Madrid. Tumejianda si kwa mechi hii tu, bali pia dhidi ya
Kenya na baadaye Nigeria ambao tutacheza nao numbani Juni 9 mwaka huu,” amesema
Phiri ambaye kwenye benchi lake la ufundi anasaidiwa na Young Chimodzi.
Viingilio katika mechi hiyo ni sh.
3,000 kwa viti vya kijani, sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000
kwa VIP C na B wakati VIP A inayochukua watazamaji 748 tu itakuwa sh. 20,000.
No comments