Header Ads

ad

Breaking News

Kawooya aitaka Klabu ya Rotary ya Bahari kuongeza wigo kusaidia jamii

Rais Mteule wa Klabu ya Rotary Club ya Bahari Dar es Salaam, Irene Bizere (kulia) akimkabidhi zawadi maalum Gavana Mkuu wa Rotary anayesimamia nchi za Tanzania na Uganda, Christine Kyeyune Kawooya (katikati). Kushoto ni Kaimu Rais wa klabu ya Klabu ya Rotary Club ya Bahari Dar es Salaam, Vipul Shah.

Na Mwandishi Wetu

UONGOZI na wanachama wa Klabu ya Rotary ya Bahari Dar es Salaam wametakiwa kupanua wigo ili kusaidia jamii katika sekta mbalimbali nchini.

Wito huo umetolewa na Gavana Mkuu wa Rotary anayesimamia Tanzania na Uganda, Christine Kyeyune Kawooya, katika mkutano maalum na wanachama wa klabu hiyo uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.

Kawooya mbali ya kuipongeza klabu hiyo kwa mchango wake mkubwa katika elimu, huduma za afya, uhifadhi wa mazingira na huduma kwa jamii, ameitaka kuongeza bidii katika masuala mbalimbali ya jamii na kuwasaidia sekta mbalimbali na kugusa maisha ya watu wengi zaidi na kuendeleza utamaduni wake wa kujitolea.

Amesema kuwa kuna umuhimu wa kuimarisha Mfuko wa Rotary (Rotary Foundation), kupitia kuongeza fedha zinazochangishwa na wanachama kwa kushirikiana na kampuni na serikali.

“Rotary Club ya Bahari imeonesha uongozi na kujitolea, lakini mahitaji bado ni makubwa. Lazima tuendelee kubuni, kushirikiana na kupanua wigo wetu kuhakikisha hakuna jamii inayosalia nyuma,” amesema.

Ameongeza kuwa, juhudi kama hizo zitawezesha klabu kukuza Rotary nchini na kufikia kiwango kingine.

“Rotary Club ya Bahari imefanikiwa kutekeleza miradi inayoshughulikia baadhi ya changamoto kubwa zaidi za kijamii,” amebainisha.

Amehimiza klabu isiishie kujikita mijini pekee, bali pia kupanua uanachama kwa kuanzisha klabu nyingi zaidi maeneo mbalimbali.

Amesisitiza klabu hiyo kuwapa kipaumbele maeneo mawili ambayo ni kupunguza vifo vya mama na watoto pamoja na kuimarisha mpango wa W.A.S.H. ambao unahisiana na udhamini wa Rotary unaosaidia miradi ya maji na usafi wa mazingira.

Amesema kuwa, Klabu ya Bahari imekuwa na mchango mkubwa katika kulea klabu nyingine za Rotary, ikiwemo Rotary Club ya Kwanza, kwa kuendeleza wakufunzi wanaoweza kufanya kazi na shule za mijini na vijijini.

“Wakufunzi hawa wamekuwa wakiwahamasisha wanafunzi kukumbatia STEAM-Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, Sanaa na Hisabati-masomo muhimu kwa kuwaandaa vijana wa Tanzania kwa maisha ya baadaye.

Miongoni mwa miradi mikubwa ni Mradi wa STEAM, ambao tayari umefikia wanafunzi zaidi ya 800 jijini Dar es Salaam na Zanzibar.

Kupitia mafunzo ya walimu na 'bootcamps,' mradi huu umewahamasisha vijana kuchunguza fursa za kazi katika sayansi na teknolojia huku ukiwapa ujasiri na stadi za kushindana katika dunia inayobadilika haraka.

Amesema Rotary Bahari imeacha alama katika afya. Mradi wa You and Me for Her wa uhamasishaji kuhusu saratani ya shingo ya kizazi umehusisha zaidi ya wanaojitolea 40, waliotoa elimu, kuhamasisha uchunguzi na kushajiisha chanjo kwa ajili ya kugundua mapema na kuzuia ugonjwa huo.

“Zaidi ya hapo, mpango wa Rotary Family Health Day umeimarisha mchango wa klabu hiyo katika afya ya jamii kwa kutoa huduma zaidi ya 10,000 kwa wanajamii 1,022.

Afya ya mama na mtoto inaendelea kuwa kipaumbele cha juu. Mradi wa Tricycle Ambulance, ambao tayari unafanya kazi, unakabiliana na changamoto za usafiri kwa kina mama wajawazito katika maeneo yenye uhitaji mkubwa.

Kufuatia mafanikio hayo, klabu sasa inapanga kuzindua motorbike ambulances chini ya Ambulance Access Initiative, mradi unaotarajiwa kunufaisha zaidi ya kina mama na watoto wachanga 5,000 kwa mwaka.

Kwa upande wake, Rais mteule wa Rotary Club ya Bahari, wakati wa ziara hiyo, Irene Bizere alisema miradi mingi ya klabu hiyo imezingatia mahitaji ya jamii, huku ikilenga zaidi mabadiliko halisi katika maisha ya watoto na wanawake.

Amesema kuwa wanajivunia kufanikisha miradi mingi pamoja na kutambua kuwa wanakazi kubwa mbele yao kutokana na mahitaji.

“Rotary Bahari imejizatiti kuongeza juhudi katika elimu ya STEAM, afya ya mama na mtoto, na uhifadhi wa mazingira. Tunataka kuhakikisha kila mradi tunaoufanya ni endelevu na unaacha athari ya kudumu.”

Kwa kuunga mkono dira hiyo, klabu imewekeza pakubwa katika uhifadhi wa mazingira. Imeotesha miti 1,360 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuzindua miradi ya 'micro-forest' shuleni.

Miradi hiyo, Gavana Kawooya alibainisha, “inaonesha dhamira ya Rotary kwa ustawi na maisha bora ya vizazi vijavyo.”

Elimu inabaki kuwa nguzo kuu ya klabu hiyo. Miongoni mwa miradi yake muhimu ni udhamini wa Shilingi milioni 5 wa maji wa Rotary, unaounga mkono programu ya Shahada ya Uzamili katika Maji na Usafi wa Mazingira.

“Udhamini huu unaonesha jinsi Rotary inavyoweza kuchangia katika kukuza uwezo wa muda mrefu kwenye sekta muhimu,” amesema Gavana Kawooya.

Rotary Club ya Bahari imebainisha vipaumbele vinne vikuu kwa mwaka huu, Ambulance Access Initiative kwa kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto na STEM Train-the-Trainer Program kwa kuwawezesha walimu.

Kampeni ya upandaji miti shuleni na kwenye jamii na Mradi wa Incinerator katika Shule ya Msingi Tuangoma, unaonufaisha wanafunzi zaidi ya 3,000 wakiwemo 35 wenye ulemavu.

Kwa uanachama imara na historia ya huduma zenye athari tangu ilipoanzishwa mwaka 1988, Rotary Club ya Bahari inaendelea kujitokeza kama moja ya klabu zenye ushawishi mkubwa zaidi nchini Tanzania, ikibaki mwaminifu kwa kaulimbiu ya Rotary ya “Service Above Self – Huduma Zaidi ya Nafsi.”

No comments