DKT. MWINYI AWAFADHILI WANAFUNZI 200 KUJIUNGA NA CHUO CHA FURAHIKA
Makamu Mkuu wa Chuo Cha Ufundi Furahika kilichopo Buguruni Malapa jijini Dar es Salaam, Dkt David Msuya,
Na Mwandishi Wetu
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imewafadhili wanafunzi 200 kujiunga na Chuo Cha Ufundi Furahika kilichopo Buguruni Malapa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuchukua kozi mbalimbali zinazofundishwa chuoni hapo.Kwa mujibu wa Makamu Mkuu wa chuo hicho, Dkt David Msuya, amesema wanafunzi hao watasoma kozi ya ushonaji, hoteli, ususi, upambanaji, makeup na nyinginezo kwa lengo la kujiajiri au kuajiliwa pindi watakapohitimu mafunzo hayo.
Mkuu wa chuo hicho leo Novemba 11, 2024 mbele ya waandishi wa habari na kufafanua kuwa, chuo hicho kina wanafunzi zaidi ya 400 wengine wakitokea Tanzania Bara wakiwa wanasoma kozi mbalimbali.
“Kwa kipekee namshukuru sana na kumpongeza Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt.Hussein Ali Mwinyi na serikali yake kwa kuthamini vijana waliotoka katika mazingira magumu na kuwaleta hapa ili wapate elimu itakayowawezesha kujikwamua kichumi na kuachana na utegemezi kutoka kwa wazazi ama walezi wao,” amasema.
Ameongeza kwamba, wanachotakiwa wanafunzi hao ni kusoma kwa bidii ili kutoiangusha serikali ambayo imejitolea kuwafadhili ili wafikie malengo yao ya kupatia ujuzi utakaowafaa maishani.
“Hizi fedha ambazo Rais Dkt. Mwinyi amezitoa kwa ajili ya kuwafadhili wanafunzi hawa zingeweza kwenda kufanya shughuli nyingine, lakini amezitoa kwao ili waweze kujikwamua kielimu na kuweza kujitegemea, wanachotakiwa ni kusoma kwa bidii ili watimize ndoto zao ambazo zilionekana kuanza kupotea,” amesema.
Pia, Dkt Msuya hakusita kumpongeza Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii, Zanzibar kwa kuonesha ushirikiano na chuo hicho na kuhakikisha vijana wanapata ujuzi na kujitegemea.
Toafuti na hilo, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kukiamini chuo hicho na kufungua milango kwa vijana ambao ndoto za kuendelea na elimu zilitoweka, lakini kupitia chuo hicho wamepata tumaini jipya katika maisha yao.
Kwa upande mwingine, Dkt. Msuya ametoa wito wa wazazi na walezi kupeleka vijana wao katika chuo hicho ili kupata ujuzi bure kupitia fani wazitakazo ikiwemo udereva, umeme na nyingine na tayari dirisha la usaili limefunguliwa.
“Niwaombe wazazi na walezi bila kujali itikadi ya dini wala siasa wawalete watoto wapate ujuzi hapa, elimu ni bure na tuna kozi nyingi ambazo mtoto akitoka hapa ataweza kujiajiri na kuajiriwa,”amesema.
Aidha, ameongeza kuwa wameongeza kozi ya Tehama lakini pia wanatarajia kuanzisha kozi ya ufundi wa pikipiki ili kuhakikisha wanamgusa kila kijana ili waweze kujitegemea.
Mwanafunzi, Safia Hamis Mwinyi, kutoka Zanzibar, ameishukuru Serikali ya Mapinduzi kwa kuwafadhili na anaamini elimu hiyo itawasaidia kujikwamua kiuchumi na kuwaondoa kwenye utegemezi na kuwasaidia wazazi wao.
No comments