Header Ads

ad

Breaking News

Ridhiwani aipongeza timu ya Best Kid ya Msata

                                         Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete

Na Omary Mngindo, Chalinze

NAIBU Waziri wa Utumishi Ridhiwani Kikwete (Mbunge) Chalinze ameipongeza timu ya soka ya Best Kid ya Msata kwa kuwa bingwa wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani.

Ridhiwani ametoa pongezi hizo baada ya kukabidhi seti ya jezi kwa timu hiyo inayojiandaa na Ligi Daraja la Tatu Mkoa wa Pwani, ikiwemo michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC), inayotarajia kuanza wakati wowote.

Ridhiwani amesema ushindi wa Best Kid wilayani humo umeleta faraja kwa Halmashauri ya Chalinze, huku akielezea juhudi za ujenzi wa uwanja wa kisasa wa michezo ulioanza kujengwa katika Kijiji cha Msoga, utaochukuwa watazamaji 10,000.

"Leo tumeanza na jezi, hapo baadaye tutakuja na mpira na mambo mengine yatafuata, halmashauri imeanza ujenzi wa uwanja pale Msoga, tunategemea kwamba, Kid wakifanikiwa utakuwa uwanja wao wa nyumbani, uwanja ule ni wa Chalinze yote," amesema Ridhiwani.

Diwani wa Kata ya Msata, Selestine Semiono 'Cham', amesema timu hiyo imepania kuipaisha Chalinze katika soka, huku akizitaka klabu nyingine kufuata nyayo hizo.

"Nichukue nafasi hii kumpongeza Mbunge wetu Ridhiwani Kikwete kwa mchango wake mkubwa kwa vijana wetu wa Best Kid na kuweza kufikia hatua hii ya kuwa bingwa wa wilaya, haya ni mafanikio makubwa kwa timu yetu na halmashauri yetu," amesema Cham.

Amesema kwamba, wataendelea kujipanga kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri zaidi kwenye Ligi Ngazi ya Mkoa ili iweze kucheza ligi ya Taifa, huku akiwapongeza kocha wa timu hiyo, Mussa Ndyamkama, nahodha, wachezaji na wana Msata.

Kocha Ndyamukama amewapongeza wakazi wa Msata kwa ushirikiano walioipatia timu yao kwa kipindi chote cha mashindano, huku akisema kwamba, walipambana kadri ya uwezo wao. 

"Nawashukuru sana wana Msata wakiongozwa na Diwani Cham, viongozi wa chama na serikali akiwemo Mkuu wa Kituo cha Polisi Msata, ambapo kwa umoja wao tumefanikisha kupatikana kwa mafanikio haya," amesema Ndyamkama.


No comments