Header Ads

ad

Breaking News

Stamico yaongeza mapato, Balile awapa ushauri

Na Mwandishi Wetu

MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, ameshauri Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), kupeleka ujuzi wake katika mashirika mengine ya serikali baada ya kupata mafanikio makubwa kiutendaji.

Balile ametoa kauli hiyo Agosti 28,2023, jijini Dar es Salaam, wakati STAMICO lilipokutana na wahariri kuelezea safari ya shirika hilo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1972.

Mwenyekiti huyo wa TEF, ameuomba uongozi wa STAMICO kujali maslahi ya wafanyakazi wao ambao ndiyo wenye kuleta mafanikio.

STAMICO limefanikiwa kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani kutoka shilingi bilioni 1.3 kwa mwaka 2018/19 hadi shilingi bilioni 61.1 kwa mwaka 2022/23, huku Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse, akisema tangu kuanzishwa kwa shirika hilo mwaka 1972, lilikuwa halipeleki kitu chochote serikalini.

Amesema tangu wapate mafanikio hayo, shirika hilo limefanikiwa kulipa gawio serikalini la shilingi bilioni 8.

Dkt.Mwasse amesema  shirika hilo lilikuwa linakwenda kufutwa, lakini kuwezeshwa na Serikali ikiwemo kubadili muundo wa shirika, ndiyo sababu iliyolifanya kufika hapo lilipo.

Ameweka wazi mikakati ya shirika hilo ikiwemo kuondoa utegemezi wa mishahara kutoka serikalini kuanzia mwaka wa fedha 2024/25.

Amesema wana mipango ya kuanzisha benki ya wachimbaji wadogo itakayosaidia kuwaondolea kero ya kutokopesheka.

Dkt. Mwasse amesema Stamico imenunua mitambo mitano ya uchorongaji itakayowasili nchini Septemba mwaka huu.

Dkt.Mwasse amesema ilifika wakati ilibidi wabadilike kifikra, kwani yapo mashirika ya umma ambayo yanatoa huduma na mengine yanatakiwa kujiendesha yenyewe.

"Tuliamua kujiendesha kibiashara, tukaanza kutafuta fursa, tulipoingia kwenye mfumo huo tukaona mambo yanakwenda vizuri,"amesema.

Amesema kwasasa wanaendelea kuzalisha kwa wingi mkaa mbadala ambao utaondoa matumizi ya kuni ns mkaa unaotokana na miti.

Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema kuwa, shirika hilo hivi sasa linafanya vizuri katika shughuli ya uchorongaji madini nchini, huku ufanisi wao ukiwawezesha kusaini mkataba wa kuchoronga na mgodi wa Geita Gold Mine (GGML), uliopo mkoani Geita.

Amebainisha kuwa, mkataba huo una thamani ya shilingi bilioni 55.2, ulisainiwa Machi 27,2023, hivyo ni uthibitisho kuwa, watanzania wanaweza kushiriki kikamilifu katika kandarasi zinazotokea kwenye madini.

Dkt.Mwasse amesema kuwa, wataendelea kuwapa mafunzo wachimbaji wadogo na kuwarasimisha kabisa, lakini wakihakikisha benki ya wachimbaji ikianzishwa ili kuwaondolea changamoto.

Amesema mbali na kuwaunganisha na benki nyingi, lakini anaamini benki ya wachimbaji madini itakuwa mkombozi mkubwa kwao.



No comments