MBUNGE ZA WANYAMA ZA KUTEMBELEWA BURE ZATAJWA?
Siku ya
Jumatatu ya Juni 5 itakuwa ni maadhimisho ya ‘Siku ya Mazingira Duniani’
ambayo huadhimishwa na mataifa tofauti duniani ikiwa imebeba kauli mbiu
ya ‘Kuwaunganisha Watu na Mazingira Asilia.’ 

Mapema
wiki hii Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia
Muungano na Mazingira, Mh. January Makamba alitoa taarifa kwa umma kuwa
kwa hapa nchini maadhimisho ya siku hiyo kitaifa yatafanyika kijijini
Butiama mkoani Mara, mahali alipozaliwa mwasisi wa taifa la Tanzania,
Hayati Mwalimu Julius Nyerere, ikiwa ni kuenzi jitihada zake za kulinda na
kuhifadhi mazingira.

Katika
kunogesha sherehe hizo Waziri huyo amesema kuwa serikali imetoa ofa kwa
wananchi kutembelea hifadhi yoyote ya mbuga ya wanyama bila ya kiingilio
chochote kwa siku tatu, kuanzia Ijumaa ya Juni 2 mpaka Jumapili ya Juni
4. Alisema kuwa lengo kubwa ni kuona uwepo wa wanyama na kujifunza kuwa
mazingira yanahitaji kulindwa zaidi na zaidi.

Kauli
hiyo ya Waziri imekuja siku chache baada ya kampuni inayojihusisha na
masuala ya huduma za hoteli mtandaoni barani Afrika, Jumia Travel
kuzindua kampeni ya ‘DemocratizeTravel’ inayolenga kuwakomboa waafrika
na watanzania kiujumla katika kusafiri na kutalii vivutio mbalimbali
nchini huku wao wakirahisisha huduma za malazi na hoteli.
Kampuni
hiyo inalenga kuhamasisha na kutoa elimu juu ya dhana potofu
iliyojengeka miongoni mwa wananchi ya kwamba mchakato mzima unaohusisha
utalii ni gharama. Katika kulifanikisha hilo kampuni hiyo imedhamiria
kuelimisha juu ya vivutio vilivyopo nchini, masuala ya msingi ya
kuzingatia wakati wa kusafiri pamoja na kurahisisha gharama za malazi
kupitia hoteli za kila hadhi zilizopo kwenye mtandao wao wa
travel.jumia.com.

Baadhi ya
changamoto zilizopo ni pamoja na mwamko mdogo wa watanzania kutembelea
vivutio vya kitalii vilivyopo karibu na wanayoishi. Wapo baadhi yao
hawafahamu kuwa wanaishi na vivutio hivyo na wengine huchukulia mchakato
mzima unahusisha gharama kubwa.
Vifuatavyo
ni baadhi ya vivutio vya kitalii ambavyo watanzania mahali popote
walipo wanaweza kwenda kuvitembelea wikendi hii bure kabisa kwa mujibu
wa kauli ya serikali katika kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani.
Kanda ya
Kaskazini. Mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Mara kwa kiasi
kikubwa imebarikiwa kuwa na hali ya hewa nzuri inayowavutia watalii,
hifadhi za mbuga za wanyama, maeneo yenye masalia ya kale pamoja na
milima ya kuvutia. Vivutio vinavyopatikana huko ni kama vile; Hifadhi za
Taifa za Arusha, Mkomazi, Ziwa Manyara, Mlima Kilimanjaro, Serengeti na
Ngorongoro. 

Kanda ya
Magharibi. Eneo hili inapatikana mikoa kama vile ya Kigoma na Rukwa
ambayo nayo haijaachwa nyuma kwa upande wa vivutio vya kitalii. Wananchi
wanaoishi katika au karibu na mikoa hii wanaweza kutembelea Hifadhi za
Mbuga za Wanyama kama vile; Gombe, Katavi, Mahale, Rubondo na Saanane na
kujionea wanyama wengi hususani sokwe wa kipekee.
Kanda ya
Kusini. Morogoro, Iringa, Mbeya na Ruvuma ni baadhi ya mikoa inayoweza
kupatikana katika ukanda huu ambapo kuna hifadhi za kitaifa kama vile;
Kitulo, Mikumi, Ruaha na Udzungwa. Mbuga kama vile Mikumi inajulikana
kuwa na idadi kubwa ya wanyama kama vile pundamilia, nyati na tembo.

Kanda ya
Mashariki. Ukanda huu kwa kiasi kikubwa umepakana na fukwe ya bahari ya
Hindi ambayo inapatikana kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani,
Lindi na Mtwara. Mbali na kuwa na hoteli nyingi zilizojengwa pembezoni
mwa fukwe ya bahari hiyo lakini pia mikoa hiyo inavyovivutio vingine
lukuki kama vile; Hifadhi ya Taifa ya Saadani, Mji wa Bagamoyo, Kisiwa
cha Kilwa, Mapango ya Amboni na Mikindani.
Visiwa
vya Zanzibar. Hakuna anayeweza kubisha kuwa vivutio mbalimbali vilivyomo
visiwani humo hususani fukwe nyingi safi na za kuvutia pamoja na hoteli
za kifahari ndivyo huwatoa watu kutoka mataifa mbalimbali duniani
kwenda kuzuru. Mbali na visiwa hivi kusifika kuwa na sehemu nzuri za
kupumzika bali pia vina utajiri mkubwa wa tamaduni za watu wa mataifa
mbalimbali waliopata kuishi humo kama vile Waarabu, Waingereza pamoja na
waafrika kwa ujumla. Lakini pia kuna majengo ya kale yaliyojengwa karne
nyingi zilizopita ambayo mpaka leo hii bado yapo na vinginevyo vingi.

Uzuri wa
nchi ya Tanzania umebarikiwa kuwa na vivutio vya kila namna karibuni
kila mkoa. Hivyo kisingizio cha kutotembelea sehemu fulani kwa sababu
ipo mbali kinakuwa hakina mantiki, Jumia Travel inakushauri anza kwanza
na vilivyo karibu nawe na fursa hii iliyotolewa na serikali inaweza kuwa
ni mwanzo mzuri kwako.
No comments