Header Ads

ad

Breaking News

Mikataba ya madini, gesi, mafuta kupitiwa na timu ya wataalam kabla ya kusainiwa

Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene (kulia) akifungua  warsha kuhusu Dira ya Madini Afrika  iliyokutanisha wataalam kutoka   taasisi za serikali nchini lengo likiwa ni kuwapa uelewa juu  ya sekta ya madini na usimamizi wa mikataba. Katikati ni Kamishna Msaidizi wa Nishati Jadidifu na Mbadala Mhandisi Edward Ishengoma. Kushoto ni mtaalam kutoka  Kitengo cha  Nishati na Mabadiliko ya Tabia Nchi, Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Abbas Kitogo. 
Mtaalam kutoka  Kitengo cha  Nishati na Mabadiliko ya Tabia Nchi, Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Abbas Kitogo akielezea mkakati wa shirika la UNDP katika kuwajengea uwezo wataalam kutoka taasisi za Serikali kuhusu usimamizi wa mikataba kuhusu madini, gesi na mafuta katika warsha hiyo. 
Washiriki  wa warsha kuhusu Dira ya Madini Afrika wakifuatilia kwa makini  hotuba ya ufunguzi iliyokuwa inatolewa na Waziri wa Nishati na Madini, George  Simbachawene (hayupo pichani). 
Waziri wa Nishati na Madini, George  Simbachawene (watatu kushoto waliokaa mbele) akiwa katika picha ya pamoja  na washiriki wa mafunzo kuhusu  Dira ya Madini Afrika iliyofanyika mjini Morogoro tarehe 21 Septemba, 2015. 
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene (kulia) akifungua  warsha kuhusu Dira ya Madini Afrika  iliyokutanisha wataalam kutoka   taasisi za serikali nchini lengo likiwa ni kuwapa uelewa juu  ya sekta ya madini na usimamizi wa mikataba. 
Kaimu Mkurugenzi wa Mikataba kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Evelyne Makala akisisitiza jambo kwenye mafunzo  hayo. 
Mafunzo yakiendelea. 
Sektretarieti  ikifuatilia kwa makini mada mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa kwa nyakati tofauti. 
Mratibu wa Mradi wa Biofueli, Wizara ya Nishati na Madini, Paul Kiwele, ( wa kwanza kushoto mbele) Kamishna Msaidizi wa Madini- Uchenjuaji na Uongezaji  Thamani  Madini, Mwacha Mtoro ( wa pili kutoka kushoto, mbele) pamoja na washiriki wengine wakifuatilia kwa makini mada mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa.

Greyson Mwase, Morogoro
 
ILI kuhakikisha kuwa  wananchi wa Tanzania wananufaika  na   rasilimali  za madini  mbalimbali pamoja na  gesi iliyogunduliwa kwa wingi hivi karibuni, Serikali imeanza kutoa mafunzo kwa wataalam kutoka taasisi za serikali watakaohusika na  upitiaji wa mikataba yote ya  shughuli za  utafutaji na uchimbaji wa  madini, gesi na mafuta kabla ya kusainiwa.

Hayo yalisemwa na  Waziri wa Nishati na Madini, George  Simbachawene  katika uzinduzi wa warsha  kuhusu dira  mpya ya madini  Afrika iliyofanyika mjini  Morogoro.

Warsha hiyo ya siku tatu iliyoandaliwa na Wizara ya Nishati na Madini ilikutanisha  wataalam kutoka  taasisi za serikali ikiwa ni pamoja  na Ofisi  ya Makamu wa Rais,  Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara  ya  Fedha, Ofisi ya Rais- Tume  ya Mipango, Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) na  Taasisi  ya  Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF).

Pia  ilikutanisha wataalam kutoka Wizara ya  Nishati na Madini pamoja na taasisi zake kama   vile Wakala wa Ukaguzi wa Madini  Nchini (TMAA), Shirika la Madini la  Taifa (STAMICO),  Shirika la Uendelezaji Nishati ya Jotoardhi Tanzania (TGDC), Mpango wa Kuongeza Uwazi na Uwajibikaji katika Tasnia ya Uziduaji  Nchini (TEITI), Mamlaka ya Udhibiti  wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Chuo cha Madini Dodoma (MRI).

Simbachawene alisema uundaji wa timu ya wataalam mbalimbali kwa ajili ya kupitia mikataba ya madini, gesi na mafuta  ni moja ya makubaliano katika utekelezaji wa Dira ya Madini  ya  Africa (Mining Vision for  Africa)  iliyoasisiwa na wakuu wa nchi zenye madini katika mkutano wake uliofanyika mwaka  2009.

Alisema kuwa katika kuhakikisha kuwa sekta ya madini inachangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi za Afrika zinazozalisha madini  wakuu wa nchi walikubaliana kuanzishwa kwa  Dira ya Madini itakayowezesha  sekta ya madini katika nchi wanachama kuboreshwa na kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Alisema kuwa katika utekelezaji wa Dira ya Madini ya Afrika, nchi  ya  Tanzania imeanza kutoa mafunzo kwa wataalam mbalimbali katika  taasisi za Serikali katika  upitiaji wa mikataba hususan  ya  utafiti na uchimbaji wa rasilimali za madini, gesi na mafuta.

Alisisitiza kuwa mara baada ya wataalam hao kupata mafunzo  wataweza kupitia mikataba mbalimbali kabla  ya kusainiwa.

“Ieleweke kwamba  suala la mikataba litakuwa si  kati ya watu wawili bali wataalam watashirikishwa kwa kupitia mikataba hiyo na kutoa mapendekezo yao kabla ya mikataba kusainiwa na Waziri ambaye ni msimamizi wa sekta husika,” alisisitiza  Simbachawene.

Akielezea ushirikishwaji wa wananchi katika usimamizi wa  sekta za madini, gesi na mafuta, Simbachawene alisema kuwa  Serikali  imehakikisha kuwa  mikataba yote inalenga kuwanufaisha wananchi kwa kushirikishwa katika utoaji wa huduma katika sekta husika.

Akitolea mfano wa  sekta ya gesi nchini, alisema fursa za utoaji wa huduma zipo nyingi na kuwataka wananchi kuchangamkia  fursa hizo
Hata hiyo alieleza kuwa Serikali  ina mkakati wa kutoa mafunzo kwa wanachi kuhusu uzalishaji wa bidhaa bora ili ziendane na soko la kimataifa.

“Tunataka ifike mahali makampuni yanayofanya  shughuli za utafiti na uchimbaji wa madini, gesi na mafuta yanunue huduma na bidhaa kwa wananchi  wa Tanzania badala ya kuagiza kutoka nje ya nchi,” alisisitza Simbachawene.

Naye mtaalam kutoka  Kitengo cha  Nishati na Mabadiliko ya Tabia Nchi, Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Abbas Kitogo alisema kuwa  shirika la UNDP limekuwa likishirikiana na Serikali katika utoaji wa mafunzo kuhusu sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na  usimamizi wa mikataba.

Alisema sekta nyeti kama za madini, gesi na mafuta zisiposimamiwa kikamilifu zinaweza kuibua migogoro badala ya kuleta maendeleo.
Alisisitiza kuwa kupitia mafunzo hayo wataalam kutoka  taasisi za serikali wataweza kupitia mikataba  mbalimbali  ya utafiti na uchimbaji wa madini, gesi na mafuta na kuishauri  serikali  kabla ya kusainiwa ili kutumika  rasmi.

No comments