MAWAKILI RUKSA RUFANI ZA UCHAGUZI TFF
WAOMBAJI uongozi kuwania nafasi mbalimbali katika
uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Kuu (TPL
Board) waliokata rufani kupinga kuenguliwa kwenye kinyang’anyiro hicho
wanaruhusiwa kuwa na uwakilishi wa kisheria (legal representation) wakati wa
kusikilizwa rufani zao.
Uamuzi wa kuruhusu mawakili kwenye usikilizaji wa rufani
hizo mbele ya Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF inayoongozwa na Idd Mtiginjola
ni kuhakikisha kila upande unapata haki.
Pia Kamati ya Uchaguzi ya TFF ambayo ndiyo iliyosaili
waombaji uongozi, hivyo kuwa mlalamikiwa katika rufani hizo, nayo inaruhusiwa
kuwa na Wakili wakati wa usikilizaji wa rufani hizo.
Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliwaengua waombaji kumi na
mbili wa uongozi kwenye nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo utakaofanyika
Februari 24 mwaka huu jijini Dar es Salaam kwa kutokidhi matakwa ya kikatiba.
Uchaguzi wa TPL Board utafanyika Februari 22 mwaka huu jijini Dar es
Salaam.
Waombaji hao waliochujwa ni Omari Mussa Nkwarulo
aliyeomba kuwania urais na Michael Richard Wambura aliyejitosa katika
kinyang’anyiro cha nafasi ya Makamu wa Rais.
Wengine waliochujwa wakiomba kugombea nafasi ya ujumbe
wa Kamati ya Utendaji ni Abdallah Hussein Musa, Mbasha Matutu, Charles Mugondo,
Ayubu Nyaulingo, Nazarius Kilungeja, Eliud Peter Mvella, Farid Nahdi, Omari
Isack Abdulkadir na Shafii Kajuna Dauda.
Kwa upande wa uchaguzi wa Bodi ya Ligi Kuu aliyechujwa
ni Christopher Peter Lunkombe aliyekuwa akiomba nafasi ya ujumbe katika Kamati
ya Uendeshaji.
Mwisho wa kukata rufani kwa waombaji uongozi
walioenguliwa na wale walioweka pingamizi kwa wagombea na zikatupwa ni leo
(Februari 7 mwaka huu) saa 10 kamili jioni.
MECHI YA STARS, CAMEROON YAINGIZA MIL
148/-
Pambano la kirafiki la kimataifa kati ya Tanzania (Taifa
Stars) na Cameroon (Indomitable Lions) lililochezwa jana (Februari 6 mwaka huu)
na wenyeji Stars kuibuka na ushindi wa bao 1-0 limeingiza sh.
148,144,000.
Fedha hizo zimepatikana kutokana na watazamaji 23,092
waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo kwa kiingilio cha sh. 5,000, sh. 7,000,
sh. 10,000, sh. 20,000 na sh. 30,000.
Mgawanyo wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; asilimia
18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni sh. 22,598,237.29, maandalizi ya
mchezo sh. 58,000,000 wakati wa gharama za uchapaji tiketi ni sh.
7,340,900.
Nyingine ni bonasi kwa wachezaji wa Taifa Stars sh.
18,831,864.41, asilimia 20 ya gharama za mchezo sh. 8,274,659.66, asilimia 15 ya
uwanja sh. 6,205,994.75 na asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika
(CAF) sh. 2,068,664.92.
Asilimia 60 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) sh. 24,823,978.98 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA)
sh. 1,241,199 ambayo ni asilimia 5 kutoka kwenye mgawo wa TFF.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF)
No comments