Serengeti Boys yaitwa Mbeya
Serengeti Boys |
TIMU ya taifa ya vijana umri chini ya miaka 17, ‘Serengeti
Boys’, imeondoka jana kwenda mkoani Mbeya kwa mwaliko wa Chama cha Soka mkoani
humo (MUFA), ikiwa ni maandalizi ya mechi ya kufuzu fainali za vijana za Afrika
zitakazofanyika mwakani nchini Morocco.
Awali, Serengeti Boys ilitakiwa kucheze na
Kenya, mechi ya kwanza, lakini timu hiyo ilijitoa kushiriki michuano hiyo.
Akizungumza jana jijini Dar Salaam, Ofisa
Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema kuwa, MUFA
wataihudumia timu hiyo kuanzia malazi, chakula na huduma nyingine ndogondogo
mpaka itakaporejea Dar es Salaam, kuendelea na kambi.
Alisema Serengeti Boys iliyo chini ya Jakob
Michelsen akisaidiwa na Jamhuri Kihwelu ‘Julio’, ipo katika maandalizi ya mechi
dhidi ya timu ya taifa ya vijana ya Misri.
Wambura alisema kuwa, timu itapangiwa
michezo ya majaribio na timu za mkoani humo, ikiwemo Mbeya City, Tanzania
Prisons na kombaini.
Aliongeza kuwa, TFF inatoa shukrani na
pongezi kwa MUFA, kwa kuonesha mfano wa kuigwa na wadau wengine wa michezo,
kushirikiana katika maandalizi ya kuziandaa timu za taifa.
“Napenda kuchukua nafasi hii kutoa
shukrani za dhati kwa MUFA, na kuwasihi wadau wenginne wa soka nchini kuiga
mfano huo kwa kuzisaidia timu zetu za taifa, kwani kufanya hivyo, tutaonesha
uzalendo, uwajibikaji na kuguswa katika masuala haya,” alisema Wambura.
Wambura aliishukuru benki ya NMB kwa kutoa
msaada wa vifaa vya michezo na fedha sh. milioni 5, ambazo zimewawezesha vijana
wa timu hiyo kupata posho zao za kambi na usafiri wa kwenda Mbeya.
Alisema kuwa, Benki ya NMB imekuwa na
mchango mkubwa katika soka la vijana kwa muda mrefu, na kwa kipindi cha miaka
sita iliyopita, ilidhamini mafunzo ya makocha wanaojihusisha na maendeleo ya
soka kwa vijana nchini.
No comments