Kamati ya utendaji ya Simba yatoa tamko
TAARIFA KWA VYOMBO VYA
HABARI
KUFUATIA maamuzi ya kikao cha
Kamati ya Katiba na Sheria ya TFF kilichokaa Jumatatu iliyopita kujadili hatma
ya wachezaji Kelvin Yondani na Mbuyu Twite, Kamati ya Utendaji ya Simba SC
ilikutana kwa siku mbili mfululizo (Septemba 11 na 12) kujadili kuhusu maamuzi
hayo.
Kabla ya kutangaza maamuzi ya
Kamati ya Utendaji, nitumie nafasi hii kuwashukuru wanachama waandamizi wa
klabu; Mzee Samuel Sitta, Profesa Philemon Sarungi, Mzee Yusuf Makamba na
Profesa Juma Kapuya kwa mchango wao mkubwa wa kimawazo kwa kamati ya utendaji
ambao ulikuwa na ushawishi mkubwa kwenye kufikia maamuzi ambayo tumeyafikia.
Kamati ya Utendaji ya Simba
imefikia maamuzi yafuatayo.
- Simba haitajitoa kushiriki katika michuano yote inayosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Ingawa uongozi ulipata shinikizo kubwa kutoka kwa wapenzi na wanachama wake la kutaka timu ijitoe kwa kutoridhishwa na maamuzi ya kamati ya sheria, uongozi umeona ni vema timu ikashiriki ligi.
Uamuzi huu
umezingatia ukweli kwamba kujiondoa kwenye ligi usingekuwa uamuzi wa kimichezo.
Hivyo Simba itashiriki katika Ligi Kuu ya Vodacom msimu unaoanza wikiendi hii.
- Kwamba wanachama au wapenzi wote waliokuwa na nia ya kutaka kupeleka suala hili mahakamani wasitishe dhamira yao hiyo. Iwapo suala hili litapelekwa mahakamani, klabu inaweza kuathirika kwa namna nyingi ikiwamo kuzuiwa kushiriki mashindano yoyote yanayotambuliwa na TFF, CAF na FIFA.
- Kwamba uongozi wa Simba unaendelea na jitihada nyingine za kutafuta haki kwenye maamuzi hayo ya kamati.
- Uongozi unalipeleka kwenye vyombo vya dola suala la mchezaji Kelvin Yondani. Kwavile mchezaji mwenyewe amekataa kuwa hakusaini Simba, namna pekee ya kumaliza utata kwenye hili ni kulipeleka kwenye vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo vina vifaa na watu wenye uwezo wa kung’amua alama za vidole za watu.
- Uongozi wa Simba utakuwa ukitoa taarifa za mara kwa mara kila zinapokuja kuhusiana na masuala haya na unawataka wanachama na wapenzi wake kutulia wakati uongozi ukiendelea kuyashughulikia
Gazeti la NIPASHE
KATIKA gazeti la NIPASHE toleo la leo Septemba 13, 2012,
ukurasa wa mwisho kuna habari yenye kichwa cha habari; “Rage Bingwa wa
Kudanganya.”
Habari hiyo ndiyo ilikuwa habari kiongozi (lead story) ya
gazeti hilo kubwa na la kuheshimika hapa nchini.
Ndani ya habari hiyo, Mwenyekiti wa Simba, Mhe; Ismail Aden
Rage, ameelezwa kuwa ni mtu mwongo na anayependa kudanganya watu kila wakati.
Habari hizi zimemsikitisha Rage binafsi na kumfedheesha kila
mwenye kuitakia mema Simba.
Kinyume kabisa cha misingi ya taaluma ya uandishi, habari
hiyo ya NIPASHE imeandikwa pasipo kumhoji Rage mwenyewe au kiongozi yeyote wa
Simba. Simba ingeelewa kama mwandishi angeandika taarifa ile kama
wazo binafsi au makala.
Lakini kuiandika kama habari, kwa kunukuu taarifa za upande
mmoja na zenye lengo la kutaka kumdhalilisha Mwenyekiti na klabu ya Simba,
gazeti la NIPASHE limekwenda mbali sana.
Kwa mfano, gazeti hilo limeeleza “uongo” mmojawapo wa Rage
kuwa ni hatua yake ya kutangaza kuitisha Mkutano Mkuu wa wanachama baada ya
maamuzi ya Kamati ya Mgongolwa.
Gazeti hilo limedai kwamba huo ni uongo kwa vile ili
kuitisha mkutano, Mwenyekiti anahitaji idhini ya zaidi ya theluthi mbili ya
wanachama. ! Hata hivyo, Katiba ya Simba inampa Mwenyekiti ridhaa ya kuitisha
Mkutano Mkuu wa dharura wakati wowote atakapoona inafaa.
Suala la theluthi mbili linakuja wakati wanachama wanapotaka
kuitisha mkutano huo wakati uongozi ukiwa hautaki. Lakini huu umeelezwa pia
kama “uongo” wa Rage.
Ikumbukwe pia kwamba Mheshimiwa Rage ni mbunge, mwenyekiti
wa Simba na ni mtu ambaye amewahi kushikilia nyadhifa mbalimbali katika sehemu
nyeti.
Kusema kwamba mtu wa namna hii ni bingwa wa kudanganya ni
matusi kwa watu wanaomchagua kushika nafasi za heshima na wale waliowahi
kumteua kushika nafasi hizo kwa kuzingatia uchapakazi wake, ushawishi wake na
mvuto alionao kwa wananchi.
Simba haina nia, sababu wala haja ya kugombana na chombo
chochote cha habari achilia mbali NIPASHE. Hata hivyo, kwa sababu taarifa hii
imegusa hadhi ya mtu binafsi na taasisi anayoiongoza au watu wanaomwamini,
klabu ingeomba yafuatayo kutoka gazeti la NIPASHE.
Kwanza, gazeti hilo liombe radhi katika kipindi cha siku
saba kutoka leo kuhusiana na habari hizo ambazo zimemsononesha sana.
Pili, radhi hiyo iombwe kwa ukubwa uleule ambao habari ya
leo iliandikwa.
Kinyume cha hayo, Rage na Simba haitasita kutafuta njia
nyingine ya kusafisha jina na hadhi yake binafsi na hadhi ya wale ambao
wanamheshimu.
Imetolewa na
Ezekiel Kamwaga
Ofisa Habari
Simba SC
Na Patrick
Mwillongo,Bagamoyo
WAZIRI wa elimu
na Mafunzo ya ufundi ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Bagamoyo Dk Shukuru
Kawambwa amemwaga msaada wa vifaa mbalimbali vya michezo kwa madiwani wa kata
za jimbo la Bagamoyo na kusaidia udhamini wa michuano ya ‘Kawambwa Cup’ kwa
jumla ya shilingi milini28.
AKizungumza
katika hafla fupi ya kukabidhi vifa hivyo, Kawambwa alisema kuwa ameamua kutoa
vifaa hivyo kwa nia ya kuwasaidia madiwani nhao kuendesha michuano yao ya kata
ambayo inashirikisha timu kutoka maeneo mbalimbali ya kata zao
“Ndugu zangu
madiwani nimeamua mimi mwenyewe kuwasaidia kuwapa vifaa hivi kwa ajili ya
kuendesha michuano yenu katika ngazi ya kata ili muweze kuleta ushindani kwa
timu na hivyo kupata timu bora zitakazoingia katika michuano ya Jimbo ya
Mbunge”alisema Dk Kawambwa
Alisema kutolewa
kwa vifaa hivyo ni mwanzo wa maandalizi ya kuanza kwa michuano ya kombe la
‘Kawambwa Cup 2012’ na kuongeza kuwa vifaa hivyo vinajumuisha jezi,mipira na
fedha taslimu shilingi 300,000 kwa ajili ya uwezeshaji wa michuano hiyo ngazi
ya kata.
Akizungumza kwa
niaba ya madiwani wenzake,Mwenyekiti wa kamati ya Kawambwa Cup ambaye pia ni
Diwani wa kata ya Dunda Mwinyihashimu Akida alimpongeza mbunge huyo kwa
moyo wake huo wa kuendeleza michezo katika jimbo la Bagamoyo na kuwataka
wabunge wengine kuiga mambo mazuri yanayofanywa na Dk Kawambwa.
“Mheshimiwa
Mbunge kwa kweli umekuwa ni tunu kubwa kwetu na unatuonyesha wazi wewe ni
mwanamichezo wa kweli ambaye umekuwa na uchungu wa kweli mpaka kufikia hatua ya
kusaidia maendeleo ya michezo kwa kutoa vifaa mbalimbali ili kuweza kuendeleza
michezo katika jimbo letu”alisema Akida .
mwisho
No comments