Hukumu ya Yondani, Twite leo
*Klabu zaitwa TFF kutoa, kutetea hoja
HUKUMU ya wachezaji waliowekewa pingamizi na klabu
mbalimbali za Ligi Kuu Tanzania Bara, itatolewa na Kamati ya Sheria, Maadili na
Hadhi za Wachezaji itakayokutana leo jijini Dar es Salaam, huku Kelvin Yondani
na Mbuyu Twite, wakigonganisha vichwa vya wengi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari
wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema kuwa, kamati
hiyo ilikutana juzi na kuamua kuziita klabu zote zilizoweka na kuwekewa
pingamizi ili zikisilikilizwe.
“Kamati imeziita timu zote zilizoweka na kuwekewa
pingamizi ili zisiwasilishe hoja zao na zilizowekewa zijibu hoja,” alisema.
Wachezaji hao wamepingwa na Simba kwa maelezo kuwa waliwasajili,
hivyo wanastahili kuitumikia klabu hiyo kongwe nchini, badala ya kuichezea
Yanga katika msimu mpya wa ligi kuu.
Wambura alisema mpaka sasa hakuna pingamizi lolote
lililotolewa uamuzi, kwani kamati ndiyo yenye maamuzi ya mwisho, ambapo
inakutana leo chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa.
Pingamizi linalosubiriwa na mashabiki wa soka ni la
Kelvin Yondan aliyeihama Simba na kutua Yanga na Mbuyu Twite aliyetoka FC Lupopo ya DR Congo,
lakini msimu uliopita akiichezea APR ya Rwanda kwa mkopo.
Mchezaji mwingine aliyekewa pingamini na timu yake
ya zamani ni Ramadhan Chombo ‘Redondo’,
aliyesaini kuichezea Simba, akitokea Azam FC pamoja na wachezaji wote wa
kigeni wa Simba, waliowekewa pingamizi na mahasimu wao, Yanga.
Wachezaji wa kigeni waliowekewa pingamizi kwa madai
kuwa, walikuwa na leseni ya kucheza soka iliyotolewa na Shirikisho la soka Tanzania (TFF), ambao
wanaichezea Simba ni Felix Sunzu, Emmanuel Okwi, Mussa Mudde, Koman Billi
Keita, Pascal Ochieng, Daniel Akuffo, Lino Musombo na Kanu Mbiyavanga na Mtanzania
Danny Mrwanda.
Kwa upande wa Yanga, wachezaji waliopinga Mbuyu
Twite na Kelvin Yondan, ambao wanadaiwa walisaini kuichezea timu hiyo. Hata
hivyo, Yondan katika michuano ya Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame),
aliruhusiwa kuichezea Yanga.
Wakati huo huo, Wambura alisema kuwa, uongozi wa
klabu ya Simba, uliwasilisha barua ya makubadiliano na Azam FC ya kuwaachia
Redondo, kwa ada ya uhamisho wa sh. milioni 25.
Wambura alisema kuwa, baada ya barua hiyo, TFF
ilipokea barua pepe kutoka katika klabu ya Azam ikielezea suala hilo, lakini
walishindwa kuifanyia kazi, kutokana na kukosa viambatanisho muhimu vya klabu
hiyo ambavyo vinaonyesha kweni inatoka Azam.
“Azam walituandikia barua pepe kutujulisha
makubaliano yao na Simba, lakini haikukamilika, hivyo haikufanyiwa kazi mpaka
watakaporekebisha, lakini iwe kabla ya kamati kuketi,” alisema.
SuperStar lilimtafuta Ofisa Habari wa Azam FC,
Jaffar Idd, ambaye alisema kuwa, wamekubaliana na Simba na tayari wamekabidhiwa
sh. milioni 10 za utangulizi, na kuahidiwa kumaliziwa sh. milioni 15, wakati wa
mechi ya Ngao ya Jamii, Septemba 11
mwaka huu.
“Simba tumemalizana kuhusu Redondo, wametutangulia
sh. milioni 10, nyingine wametuahidi wakati wa mechi ya Ngao ya Jamii,”
alisema.
Lakini, alipoulizwa kuhusu barua pepe waliyotuma
TFF, alisema kuwa, hana maelezo zaidi ya hayo ya kukubaliana.
No comments