Maximo: nitaijenga Yanga, kutua Jumanne
![]() |
Marcio Maximo |
KOCHA wa zamani wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’
aliyewezesha kupandisha soka nchini, Marcio Maximo, amesema kuwa, ataijenga
vizuri Yanga na kuwa moja ya timu tishio barani Afrika.
Akizungumza kwa njia ya mtandao, Maximo alisema soka
la Tanzania analifahamu, hivyo ana uhakika wa kukisuka vizuri kikosi hicho na
kuleta ushindani mkubwa barani Afrika.
“Ninalijua soka la Tanzania, Afrika Mashariki na
Afrika, nina uhakika wa kufanya mambo makubwa zaidi ya yale ya Stars,” alisema.
Kocha huyo aliwahi kuifikisha katika viwango vya
soka duniani katika nafasi ya 100 bora na kuipa matumaini ya kuzidi kupanda kwa
upamnde wa viwango.
Maximo, anatarajiwa kutua nchini Jumanne ijayo kwa
ajili ya kuingia mkataba na klabu hiyo yenye maskani yake katika makutano ya
mitaa ya Twiga na Jangwani jijini Dar es Salaam.
Taarifa zilizotua kwenye dawati la SuperStar
zilisema kuwa, baada ya kuwasili kwenye
Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere, siku hiyo ya Jumanne ya Juni 12
mwaka huu, Maximo atakwenda moja kwa moja makao makuu ya klabu hiyo na kufanya
mazungumzo ya faragha na uongozi wa Yanga.
“Kocha akishawasili atakutana na uongozi kisha
atawasaliamia wanachama na wapenzi wa Yanga na baadaye atakwenda kupunzika kisha
kukutana naye kwa ajili ya kutia saini mkataba wa kuifundisha timu mbele ya
wanahabari siku inayofuata.
“Baada ya
mambo hayo kukamilika tunarajia kikosi kitaitwa na kukunana na wachezaji wote
waliosajiliwa kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, pamoja na
michuano ya Kagame ambayo Yanga ni bingwa mtetezi.
“Pia kuna safari ya kwenda Unguja na Pemba kwa ajili
ya kujiandaa na michuano hiyo ya Kagame, ambapo wanachana na wapenzi wa Yanga
watakuwa na fursa ya kuiona wakati ikiwa katika harakati zake za kuutetea
ubingwa wake,” kilisema chanzo chetu ndani ya Yanga.
Maximo, raia wa Brazil ni miongoni mwa makocha wenye
uwezo mkubwa wa kushawishi mashabiki, kitu ambacho kinaweza kumsaidia kuungwa
mkono katika majukumu yake.
Miongoni mwa majukumu atakayoanza nayo, ni
kuhakikisha Yanga inalibakiza kombe la Kagame na kuutwaa ubingwa Bara msimu
ujao.
Kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Taifa Stars,
ndiye aliyekuwa chachu ya mashabiki kukishangilia kikosi cha Stars kinapokuwa
na mechi.
No comments