WAZIRI MAKALA AIKABIDHI BENDERA TWIGA STARS
![]() |
Amos Makala |
Timu ya Taifa ya mpira wa miguu kwa
wanawake (Twiga Stars) inayotarajia kuondoka leo saa 11.05 jioni kwa ndege ya
Ethiopian Airlines kwenda Ethiopia imekabidhiwa Bendera ya Taifa na Naibu
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla.
Twiga Stars yenye msafara wa watu 24
wakiwemo wachezaji, benchi la ufundi na viongozi itacheza na Ethiopia katika
mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya michuano ya mchujo kwa ajili ya Fainali za
Nane za Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) zitakazofanyika Novemba mwaka huu
Equatorial Guinea.
Mechi hiyo itafanyika Mei 27 mwaka
huu kwenye Uwanja wa Addis Ababa wakati ile ya marudiano itachezwa Juni 16
mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Twiga Stars ikifanikiwa kuitoa
Ethiopia itakuwa imepeta tiketi ya kwenda Equatorial Guinea.
Wachezaji walioondoka na kikosi
hicho ni Amina Ally, Asha Rashid (nahodha), Ester Chabruma, Ettoe Mlenzi,
Evelyn Sekikubo, Fadhila Hamad, Fatuma Bashiri, Fatuma Khatib, Fatuma Mustafa,
Fatuma Omari, Maimuna Said, Mwajuma Abdallah, Mwanahamisi Omari, Mwanaidi
Tamba, Mwapewa Mtumwa, Rukia Hamis, Semeni Abeid na Zena Khamis.
Kwa upande wa Benchi la Ufundi ni
Charles Mkwasa (Kocha Mkuu), Nasra Mohamed (Kocha Msaidizi), Furaha Francis
(Meneja wa Timu), Mwanahamisi Abdallah (Mtunza Vifaa) na Christina Luambano
(Daktari wa Timu).
Twiga Stars ambayo msafara wake
unaongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu kwa Wanawake Tanzania
(TWFA) ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) itarejea nyumbani Mei 28 mwaka huu saa 6 mchana kwa ndege
ya Ethiopian Airlines.
No comments